Somalia yaishutumu Ethiopia kuwa inatuma silaha katika jimbo la Puntland
Somalia ilishutumu Ethiopia siku ya Ijumaa kuwa inatuma silaha ambazo hazijaidhinishwa katika jimbo lake lenye mamlaka ya ndani la Puntland.
Wizara ya Mambo ya Nje ilisema kutumwa shehena za silaha hizo ni kinyume cha mamlaka ya kujitawala Somalia na "ni tishio kwa usalama wa kikanda."
Aidha taariha ya wizara hiyo imeongeza kuwa ushahidi uliorekodiwa umethibitisha kuwasili kwa lori mbili zilizojaa silaha kutoka Ethiopia hadi eneo la Puntland nchini Somalia na kuwa silaha hizo zimeingizwa bila ushirikiano wowote wa kidiplomasia au kibali.
Madai ya kuingizwa silaha katika eneo hilo yanakuja huku mvutano kati ya nchi hizo mbili kuhusu makubaliano ya Ethiopia ya kufikia bahari na eneo lililojitenga la Somaliland ukiendelea kuongezeka.
Somalia imekataa makubaliano ya Somaliland na Ethiopia kuhusu kukodishwa nchi hiyo bandari kwa miaka 50 katika eneo la Bahari Nyekundu la Somaliland, na kuyataja kuwa tishio kwa ujirani mwema na ukiukaji wa uhuru wake.
Somalia ilimwita nyumbani balozi wake nchini Ethiopia baada ya mpango huo kutangazwa.
Uturuki hata hivyo, imekuwa ikifanya upatanishi wa kumaliza mvutano kati ya nchi hizo za Pembe ya Afrika lakini mazungumzo ya hivi karibuni mjini Ankara hayajazaa matunda.