Mtoto wa Museveni: Sina nia ya kugombea kiti cha urais 2026
Mtoto wa kiume wa Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda ametangaza leo kuwa, hana nia ya kugombea kiti cha urais na badala yake atamuunga mkono baba yake.
Muhoozi Kainerugaba ambaye wengi wanaamini anaandaliwa kwa ajili ya kumrithi baba yake, ametangaza kupitia ukurasa wa mtandao wa X kwamba hatosimama kuwania urais wa Uganda katika uchaguzi ujao.
Mtoto huyo wa rais Museveni ambaye sasa anashikilia wadhifa wa Mkuu wa Majeshi ya Uganda amesema kuwa, atamuunga mkono baba yake anayeitawala nchi hiyo ya Afrika Mashariki tangu mwaka 1986.
Kainerugaba anatangaza msimamo huo katika hali ambayo, huko nyuma amewahi kunukuliwa akisema kuwa, atawania kiti cha urais katika uchaguzi wa mwaka 2026.
Museveni mwenyewe bado hajatangaza iwapo atawania muhuka wa 7 madarakani ifikapo 2026. Kainerugaba alisema hapo kabla dhamira yake ya kuwania urais ni kuwezesha damu changa kuongoza siasa za nchi hiyo.
Mtoto huyo wa Rais Museveni amekuwa akitangaza misimamo ambayo wakati mwingine inakinzana na ile ya serikali ya Uganda na kuzusha mtafaruku katika uhusiano wa nchi hiiyo na majirani zake.
Huko nyuma Luteni Jenerali Muhoozi Kainerugaba, amewahi kunukuliwa akitangaza kuliunga mkono kundi la waasi la M23, linalopigana vita na jeshi la serikali ya Kinshasa na kueleza kwamba, lina haki ya kufanya hivyo.