Mahakama ya Kenya yataka Meta ifunguliwe mashtaka
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i116614-mahakama_ya_kenya_yataka_meta_ifunguliwe_mashtaka
Mahakama nchini Kenya imetangaza kuwa, kampuni kubwa ya mtandao wa kijamii ya Marekani, Meta, inaweza kufunguliwa mashtaka kuhusu mazingira duni ya kazi na kuachishwa kazi kwa wafanyakazi wake.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Sep 21, 2024 08:43 UTC
  • Mahakama ya Kenya yataka Meta ifunguliwe mashtaka

Mahakama nchini Kenya imetangaza kuwa, kampuni kubwa ya mtandao wa kijamii ya Marekani, Meta, inaweza kufunguliwa mashtaka kuhusu mazingira duni ya kazi na kuachishwa kazi kwa wafanyakazi wake.

Uamuzi huo wa Mahakama ya Kenya sasa unafungua njia ya mapambano ya kisheria na wafanyakazi wa zamani wa kampuni hiyo.

Uamuzi huo uliotolewa mjini Nairobi, mji mkuu wa Kenya unafuatia kutimuliwa kazini kwa wasimamizi wa maudhui kwenye mtandao wa Facebook na kampuni ya SAMA iliyopewa kandarasi ya kusimamia kazi za kampuni ya Meta nchini Kenya.

Kesi ya kwanza iliwasilishwa zaidi ya miaka miwili iliyopita na Daniel Motaung, msimamizi wa maudhui wa Afrika Kusini ambaye aliwahi kufanya kazi katika kampuni hiyo.

Kesi nyingine ilifunguliwa mwezi Machi mwaka jana (2023), ambapo wasimamizi 185 waliofukuzwa kazi na Sama wanadai kuwa walizuiwa kutuma maombi ya majukumu sawa katika kampuni nyingine.

 

Hata hivyo kampuni ya Meta ambayo mpaka sasa haijatoa tamko lolote bado inaweza kukata rufaa katika Mahakama ya Juu.

Kampuni ya Meta imewahi kuandamwa pia kwa ubaguzi na uchujaji taarifa.

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limewahi kutangaza kuwa,  sera za kampuni ya Meta zimezidi kuziba na kunyamazisha sauti zinazoiunga mkono Palestina kwenye mitandao ya kijamii ya Instagram na Facebook kutokana na vita vya Israel dhidi ya Gaza.

Ripoti ya Human Rights Watch imeeleza kwamba kuna mtindo wa kuondolewa na kufuta bila sababu maudhui zinazoiunga mkono Palestina, ikiwa ni pamoja na maudhui ya kujieleza kwa amani na mjadala wa umma kuhusu haki za binadamu za Wapalestina.