Niger yazindua kampeni ya chanjo dhidi ya Malaria
Niger imekuwa nchi ya hivi karibuni katika kanda ya Afrika Magharibi kuzindua mpango wa chanjo ya Malaria ili kujaribu kuzuia ugonjwa huo hatari.
Garba Hakimi, Waziri wa Afya wa Niger amesema wamezindua kampeni kubwa ya chanjo huku awamu ya kwanza ikifanyika katika mji wa Kusini Magharibi wa Gaya, kitovu cha ugonjwa wa malaria unaoenezwa na mbu. Kwa wastani wagonjwa wa malaria milioni tano hurekodiwa nchini Niger kila mwaka huku zaidi ya watu 5,000 wakipoteza maisha yao. Kulingana na takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), mnamo mwaka 2022, malaria ilisababisha vifo vya zaidi ya watu 600,000 duniani kote – asilimia 95 kati yao wakiwa ni kutoka barani Afrika na asilimia 80 wakiwa watoto wa chini ya umri wa miaka mitano.
WHO imesema katika taarifa yake kuwa, dawa ya kupambana na malaria RTS,S – iliyotengenezwa na kampuni ya dawa ya Uingereza ya GSK – itatumika kwenye kampeni hiyo ya chanjo nchini Niger ambayo iliidhinisha mwaka 2022.
Takwimu za Shirika la Afya Duniani zinaonesha kuwa, kwa wastani bara la Afrika linarekodi kesi milioni 200 na vifo 400,000 kwa mwaka vinavyosababishwa na ugonjwa wa malaria. Malaria husababishwa na vimelea na huambukizwa kwa binadamu kupitia mbu jike aina ya Anopheles. Ingawa ugonjwa huo unaweza kuzuilika na kutibika, unaweza kusababisha kifo usipotibiwa.