UNICEF yataka dola milioni 58.8 kukomesha mlipuko wa mpox Afrika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i116628-unicef_yataka_dola_milioni_58.8_kukomesha_mlipuko_wa_mpox_afrika
Mfuko wa Kuhudumia Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF), umetoa ombi la dharura la karibu dola milioni 59 kusaidia juhudi za kukomesha maradhi ya MPOX.
(last modified 2024-09-21T23:28:24+00:00 )
Sep 21, 2024 23:28 UTC
  • UNICEF yataka dola milioni 58.8 kukomesha mlipuko wa mpox Afrika

Mfuko wa Kuhudumia Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF), umetoa ombi la dharura la karibu dola milioni 59 kusaidia juhudi za kukomesha maradhi ya MPOX.

Taarifa ya UNICEF imeeleza kuwa, unahitajia kiwango hiicho cha fedha kwa ajili ya kukabiliana na kusambaa kwa kasi kwa ugonjwa wa homa ya nyani au mpox katika nchi sita za Afrika ikiwemo Burundi, ambako watoto wameathiriwa zaidi.

Dkt. Paul Ngwakum, Mshauri wa Afya wa UNICEF Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika amesema “Watoto nchini Burundi wanabeba mzigo mkubwa wa mlipuko wa mpox na viwango vya kutisha vya maambukizo na athari za kiafya. Amesema, kati ya karibu wagonjwa 600 walioripotiwa, theluthi mbili ni watoto walio na umri wa chini ya miaka 19 na hali inaongezeka kwa kasi kubwa ikiwa ni ongezeko la zaidi ya asilimia 40 katika wiki tatu zilizopita."

Chanjo ya MPOX

 

Kwa upande wake mwakilishi wa UNICEF nchini Burundi France Bégin amesema ongezeko la maambulizi ya mpox miongoni mwa watoto nchini Burundi wakiwemo wenye umri wa chini ya miaka mitano linatia wasiwasi mkubwa na kuwalinda ndio kipaumbele chetu.

Agosti 14 mwaka huu, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitangaza hali ya dharura ya kimataifa kutokana na kusambaa kwa virusi vya mpox, hasa kuongezeka kwa visa vya maambukizi vya aina mpya ya virusi hivyo inayofahamika kama Clade 1b nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Kwa mujibu wa WHO, kanda ya Afrika hivi sasa inashuhudia ongezeko la maambukizo ya homa hiyo, huku mataifa 14 ya bara hilo yakiathirika.

Shirika la Afya Duniani limetangaza kuwa, licha ya kuwa maambukizi ya ugonjwa huo yamekuwa yakiongezeka kwa kasi, lakini vifo vinavyotokana na maradhi hayo ni vichache.