Maandamano yafanyika Somalia kupinga wanajeshi wa Misri
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i116650-maandamano_yafanyika_somalia_kupinga_wanajeshi_wa_misri
Hatua ya Somalia ya kuwaalika wanajeshi wa Misri katika ardhi yake imeibua hitilafu kati ya serikali kuu ya Mogadishu na majimbo yake ya shirikisho, katika kile kinachoweza kuharibu mwelekeo wa nchi hiyo katika mahitaji ya usalama.
(last modified 2024-09-22T08:47:59+00:00 )
Sep 22, 2024 08:47 UTC
  • Maandamano yafanyika Somalia kupinga wanajeshi wa Misri

Hatua ya Somalia ya kuwaalika wanajeshi wa Misri katika ardhi yake imeibua hitilafu kati ya serikali kuu ya Mogadishu na majimbo yake ya shirikisho, katika kile kinachoweza kuharibu mwelekeo wa nchi hiyo katika mahitaji ya usalama.

Mamia ya watu huko Waajid, mji wa pili mkubwa katika eneo la Bakol katika Jimbo la Kusini Magharibi (SWS) la Somalia hivi karibuni waliandamana barabarani, wakiwa wamebeba mabango yenye maandishi kama vile 'doonimayno Masar' (hatutaki Misri) na 'soo dhowoow Itoobiya  (karibu Ethiopia).

Maandamano hayo yalivuruga usafiri kati ya Baidoa, mji mkuu wa Kusini Magharibi na Mogadishu huku mamlaka zikijaribu kutuliza maandamano hayo yasiyo ya kawaida.

Kutokana na hali hiyo, Waziri Mkuu wa Somalia Hamza Abdi Barre alisafiri kwa ndege hadi Baidoa akiwa na wasaidizi wakuu akiwemo Mkurugenzi wa Shirika la Kitaifa la Ujasusi na Usalama (NISA) Abdullahi Mohamed Ali almaarufu Sanbaloolshe.

Kulingana na mpango wa Somalia, Kikosi cha sasa cha Mpito cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (ATMIS) kinatazamiwa kupunguza askari wake ifikapo Desemba 31 mwaka huu.

Nafasi ya ATMIS inatarajiwa kuchukuliwa na kikosi kingine cha kulinda amani cha AU kinachoitwa Misheni ya Kusaidia na Kuimarisha Udhibiti wa Umoja wa Afrika nchini Somalia (AUSSOM), ambapo kwa mujibu wa uamuzi uliochukuliwa na serikali ya Somalia vikosi vya Ethiopia havitaruhusiwa tena kubaki nchini humo, kuanzia tarehe 1 Januari 2025.

Badala yake, wanajeshi wa Misri, wanaotarajiwa kufikia 5,000 watashiriki katika AUSSOM pamoja na wengine 5,000 zaidi wanaowasili kupitia makubaliano ya kiulinzi  kati ya Somalia na Misri.

Uhusiano kati ya Somalia  na Ethiopia ulivurugika mapema mwaka huu baada ya Ethiopia isiyo na bandari kusaini mapatano ya kukodi kilomita 20 za ukanda wa pwani ya Somaliland - sehemu ya Somalia ambayo imejitangazia uhuru na imekuwa ikijitawala tangu 1991, lakini imeshindwa kutambuliwa kimataifa.

Serikali ya Somalia ilipinga vikali mapatano hayo ya miaka 50 na imeamua kuomba msaada wa kijeshi wa Misri kukabiliana na tishio hilo la Ethiopia.