Mtoto wa Museveni: Uganda haitaongozwa na rais ambaye ni raia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i116656-mtoto_wa_museveni_uganda_haitaongozwa_na_rais_ambaye_ni_raia
Mkuu wa jeshi la Uganda, ambaye ni mtoto wa kiume wa rais Yoweri Museveni, Jenerali Muhoozi Kainerugaba amesema kwamba, hakuna raia atakayeongoza Uganda na kwamba hilo ni jukumu la wanajeshi au polisi.
(last modified 2024-09-22T09:21:22+00:00 )
Sep 22, 2024 09:21 UTC
  • Mtoto wa Museveni: Uganda haitaongozwa na rais ambaye ni raia

Mkuu wa jeshi la Uganda, ambaye ni mtoto wa kiume wa rais Yoweri Museveni, Jenerali Muhoozi Kainerugaba amesema kwamba, hakuna raia atakayeongoza Uganda na kwamba hilo ni jukumu la wanajeshi au polisi.

Muhoozi ameandika ujumbe kwenye mtandao wa X kwamba katu wanajeshi hawataruhusu raia kuongoza Uganda.

“Hakuna raia ataongoza Uganda baada ya rais Yoweri Museveni. Maafisa wa usalama hawataruhusu hilo kutokea. Raia ajaye atakuwa mwanajeshi au afisa wa polisi,” ameandika Muhoozi.

Hayo yanajiri katiika hali ambayo, mtoto huyo wa kiume wa Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda ametangaza kuwa, hana nia ya kugombea kiti cha urais na badala yake atamuunga mkono baba yake.

Muhoozi Kainerugaba ambaye wengi wanaamini anaandaliwa kwa ajili ya  kumrithi baba yake, ametangaza kupitia ukurasa wa mtandao wa X kwamba hatosimama kuwania urais wa Uganda katika uchaguzi ujao.

Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda ambaye hivi karibuni alitimiza miaka 80 amekuwa akiiongoza Uganda tangu mwaka 1986

 

Mtoto huyo wa rais Museveni ambaye sasa anashikilia wadhifa wa Mkuu wa Majeshi ya Uganda amesema kuwa, atamuunga mkono baba yake anayeitawala nchi hiyo ya Afrika Mashariki tangu mwaka 1986.

Kainerugaba anatangaza msimamo huo katika hali ambayo, huko nyuma amewahi kunukuliwa akisema kuwa, atawania kiti cha urais katika uchaguzi wa mwaka 2026.

Museveni mwenyewe bado hajatangaza iwapo atawania muhula wa 7 madarakani ifikapo 2026. Kainerugaba alisema hapo kabla dhamira yake ya kuwania urais ni kuwezesha damu changa kuongoza siasa za nchi hiyo. Mtoto huyo wa Rais Museveni amekuwa akitangaza misimamo ambayo wakati mwingine inakinzana na ile ya serikali ya Uganda na kuzusha mtafaruku katika uhusiano wa nchi hiiyo na majirani zake.