Mafuriko yaua zaidi ya watu 500 nchini Chad
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i116662-mafuriko_yaua_zaidi_ya_watu_500_nchini_chad
Zaidi ya watu 500 wanaripotiwa kupoteza maisha nchini Chad kufuatia mafuriko makubwa yaliyosababishwa na mvua kubwa nchini humo.
(last modified 2024-09-22T23:23:26+00:00 )
Sep 22, 2024 23:23 UTC
  • Mafuriko yaua zaidi ya watu 500 nchini Chad

Zaidi ya watu 500 wanaripotiwa kupoteza maisha nchini Chad kufuatia mafuriko makubwa yaliyosababishwa na mvua kubwa nchini humo.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) nchini Chad imetangaza kuwa, mvua zinazoendelea kunyesha nchini Chad tangu mwezi Julai zimesababisha vifo vya watu 503 na kuathiri zaidi ya watu milioni 1.7.

Kwa mujibu wa ripoti mbalimbali ni kuwa, "Kaunti 117 kati ya 125 zimeathirika" ambapo nyumba 212,111 na heka 357,832 za mashamba zimeharibiwa huku zaidi ya ng'ombe 69,659 zikisombwa na maji.

Marcelin Kanabé Passalé, Waziri wa Maji na Nishati wa Chad amesema, mvua hizi zimesababisha mafuriko makubwa ambayo yameathiri majimbo yote ya nchi, na kusababisha mamia ya watu kupoteza maisha lakini pia uharibifu mkubwa wa mkiuundombinu na mifugo.

 

Waziri huyo pia ametangaza kuanzishwa kwa kamati ya ufuatiliaji wa mafuriko, ili "kutathmini hatari zinazohusishwa na uchafuzi wa vyanzo vya maji ya kunywa na kupanda kwa viwango vya mito". Baadhi ya ripotii zinasema kuwa, maji ya Mto Logone na Mto Chari yamefikia kimo kikubwa ambacho kinaweza kusababisha mafuriko katika siku zijazo.

Umoja wa Mataifa ulionya mwanzoni mwa mwezi huu wa Septemba kuhusu athari za "mvua kubwa na mafuriko makubwa" katika kanda hiyo, hasa nchini Chad, na kutoa wito wa kuchukuliwa "hatua za haraka na ufadhili wa kutosha" iili  kukabiliana na "mgogoro wa hali ya hewa".