Maandamano yafanyika kote Morocco kuunga mkono Wapalestina
Zaidi ya maandamano 100 yaliandaliwa kote Morocco siku ya Ijumaa kulaani mashambulizi ya utawala wa Kizayuni wa Israel kwenye Ukanda wa Gaza na kuonyesha uungaji mkono kwa Wapalestina wanaodhulumiwa.
Wakfu wa Uungaji Ummah, kikundi cha kiraia cha Morocco, kimesema maandamano 106 yalifanyika katika miji 50.
Waandamanaji walitoa nara za kuunga mkono muqawama wa Wapalestina na kupinga vita na mashambulio ya kinyama ya utawala wa Kizayuni wa Israel huko Gaza, Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Palestina yote, pamoja na uungaji mkono wa Marekani na Magharibi kwa Israel na "kimya" cha ulimwengu wa Kiarabu.
Pia wamelaani mashambulizi ya Israel dhidi ya raia huko Lebanon, Yemen, Syria na Iraq.
Maandamano ya kila siku yanafanyika katika miji, ikiwa ni pamoja na mji mkuu wa Rabat, kutaka kusitishwa mashambulizi ya Israel, kuondolewa mzingiro, na kupelekwa misaada ya kibinadamu huko Gaza.
Tangu Oktoba 7, 2023, vita vya kinyama na mashambulizi ya Israel yameua shahidi Wapalestina 41,272 huko Gaza, wakiwemo watoto 16,795 na wanawake 11,378, na kujeruhi 95,551.
Maelfu wamesalia chini ya vifusi huku hospitali na shule zikilengwa, na kuharibiwa pia miundombinu ya kiraia.
Katika Ukingo wa Magharibi na Quds Mashariki, Wapalestina 716 wameuliwa shahidi na wanajeshi wa Israel na walowezi wa Kizayuni tangu Oktoba 7, 2023.