Watu 15 wauawa na wengine 61 wajeruhiwa katika shambulio jipya nchini Sudan
Takriban watu 15 wameuawa na wengine 61 kujeruhiwa katika shambulio la mizinga lililofanywa na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) kwenye soko lililojaa watu katika mji wa Omdurman, kaskazini mwa mji mkuu wa Sudan, Khartoum.
Mohamed Ibrahim, msemaji wa Wizara ya Afya ya Jimbo la Khartoum ametangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, majeruhi hao wamehamishiwa katika hospitali za Al-Nao na Sawaed. Amebainisha kuwa, idadi ya waliouawa inaweza kuwa kubwa zaidi kwani kikosi cha uokoaji hakiwezi kuwafikia na kuwatambua baadhi ya majeruhi.
Hadi tunapokea habari hii, kundi la RSF lilikuwa halijatoa maoni yoyote kuhusu shambulio hilo.
Tangu Aprili 15, 2023, Sudan imekuwa katika mgogoro mkubwa kati ya Jeshi la Sudan na RSF na kusababisha kwa uchache watu 16,650 kuuawa na mamilioni ya watu kuyahama makazi yao. Hayo ni kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa.
Vyombo vya habari vya jeshi la Sudan vinasema kuwa, kundi la RSF limekuwa likishambulia mara kwa mara eneo la soko la Sabreen katika siku za hivi karibuni.
Mohamed Ibrahim, msemaji wa Wizara ya Afya katika jimbo la Khartoum amesema kuwa, RSF imeshambulia soko la Sabreen huko Karari na huenda idadi ya waliouawa ikaongezeka kwani wengi wa waliojeruhiwa wako katika hali mbaya.
Mzozo wa uchu wa madaraka baina ya majenerali wa kijeshi yaani baina ya kundi la RSF, linaloongozwa na Mohamed Hamdan Dagalo "Hemetti" na Jeshi la Sudan SAF linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, tangu mwezi Aprili 2023 umeshapelekea mamilioni ya watu kuyahama makazi yao na kusababisha mgogoro mkubwa wa kibinadamu.