Burkina Faso yazima jaribio la kuyumbisha usalama wa nchi hiyo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i116758-burkina_faso_yazima_jaribio_la_kuyumbisha_usalama_wa_nchi_hiyo
Waziri wa Usalama wa Burkina Faso, Mahamadou Sana amesema kwenye televisheni ya taifa kwamba "watu wanaoishi Cote d'Ivoire wamehusika katika shughuli za uasi dhidi ya usalama wa taifa.
(last modified 2024-09-25T10:26:17+00:00 )
Sep 25, 2024 10:26 UTC
  • Burkina Faso yazima jaribio la kuyumbisha usalama wa nchi hiyo

Waziri wa Usalama wa Burkina Faso, Mahamadou Sana amesema kwenye televisheni ya taifa kwamba "watu wanaoishi Cote d'Ivoire wamehusika katika shughuli za uasi dhidi ya usalama wa taifa.

Waziri huyo amewashutumu watu 14 kwa kupanga njama hiyo ya kuhatarisha utulivu wa nchi. Miongoni mwa wapinzani wa utawala wa hivi sasa ni kiongozi wa mapinduzi ya kijeshi ya mwezi Januari 2022, mawaziri wawili wa zamani na waandishi wa habari wawili. Waliokula njama hiyo wasiojulikana ni pamoja na maafisa wa ujasusi wa nchi za Magharibi.

Maafisa wa serikali ya Burkina Faso wanasema kuwa, njama hiyo ya siri sana ya awamu tatu ilipangwa na baadhi ya raia wa Burkina Faso na wanajeshi wanaoishi nje ya nchi ambao walilipia gharama na kutoa mafunzo kwa vikundi vya kigaidi ili kuendesha njama hiyo ya mapinduzi. Wanaharakati wa uchumi na viongozi wa mashirika ya kiraia nao wanadaiwa kuhusika katika njama hizo za mapinduzi. 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, awamu ya pili ya njama hiyo ya mapinduzi ilipangwa kuwa ya mashambulizi dhidi ya ikulu ya rais, kituo cha kijeshi cha ndege zisizo na rubani na uwanja wa ndege. Awamu ya mwisho ilikuwa imepangwa kuendeshwa kwa mashambulizi karibu na mpaka wa Burkina Faso na Ivory Coast.