Waliofariki dunia kwa mripuko wa kipindupindu Sudan wameongezeka hadi watu 433
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i116760-waliofariki_dunia_kwa_mripuko_wa_kipindupindu_sudan_wameongezeka_hadi_watu_433
Idadi ya watu waliopoteza maisha katika mripuko wa kipindupindu nchini Sudan imeripotiwa kuongezeka na kufikia watu 433.
(last modified 2024-09-25T10:28:15+00:00 )
Sep 25, 2024 10:28 UTC
  • Waliofariki dunia kwa mripuko wa kipindupindu Sudan wameongezeka hadi watu 433

Idadi ya watu waliopoteza maisha katika mripuko wa kipindupindu nchini Sudan imeripotiwa kuongezeka na kufikia watu 433.

Taarifa ya Wizara ya Afya ya Sudan imesema kuwa, idadi ya walioambukizwa kipindupindu imeongezeka huku nchi hiyo ikiendelea kuteseka kwa matatizo mengine mengi yanayosababishwa na vita vya uchu wa madaraka vinavyoongozwa na majenerali wa kijeshi wanaongoza makundi mawili hasimu nchini Sudan. 

Serikali ya Sudan ilitangaza rasmi kuzuka janga la kipindupindu nchini humo tarehe 12 Agosti mwaka huu.

Mwishoni mwa mwezi Agosti, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR lilitangaza kupitia mwakilishi wake nchini Sudan, Kristine Hambrouck kwamba mripuko mpya wa kipindupindu nchini humo ambao ni wimbi la pili tangu vilipoanza vita vya uchu wa madaraka baina ya majenerali wa kijeshi.

Wananchi wa Sudan wanateseka kwa mambo mengi, vita, magonjwa n.k

 

Mbali na kuenea ugonjwa wa kipindupindu, limeripotiwa pia ongezeko la maambukizi ya magonjwa yatokanayo na maji yakiwemo malaria na kuharisha.

Imeelezwa pia kuwa, mapigano, kukosekana usalama na mvua zinazoendelea kunyesha vinatatiza usafirishaji wa misaada ya kibinadamu. Katika majimbo ya Sennar, Blue Nile, Jazirah, White Nile, Darfur na Kordofan - yanayotoa hifadhi kwa zaidi ya wakimbizi milioni saba na laki nne pamoja na wakimbizi wa ndani wa Sudan - kuna changamoto za upatikanaji wa huduma kwa kuchelewesha utoaji wa dawa muhimu na vifaa vya msaada.

Tangu vilipoanza vita na mapigano nchini Sudan, zaidi ya watu milioni kumi na laki tatu wamelazimika kuyahama makazi yao na kutafuta hifadhi ndani au nje ya nchi hiyo.