Ajali mbaya ya barabarani yaua na kujeruhi watu 37 kusini mwa Ethiopia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i116822-ajali_mbaya_ya_barabarani_yaua_na_kujeruhi_watu_37_kusini_mwa_ethiopia
Watu 28 wamepoteza maisha na wengine 19 kujeruhiwa katika ajali mbaya ya barabarani iliyotokea kusini mwa Ethiopia.
(last modified 2024-09-27T03:17:02+00:00 )
Sep 27, 2024 03:17 UTC
  • Ajali mbaya ya barabarani yaua na kujeruhi watu 37 kusini mwa Ethiopia

Watu 28 wamepoteza maisha na wengine 19 kujeruhiwa katika ajali mbaya ya barabarani iliyotokea kusini mwa Ethiopia.

Vyombo vya habari vya nchi hiyo vimetangaza kuwa ajali hiyo mbaya imetokea wakati basi lililokuwa likisafiria kutoka Wolaita Sodo kwenda eneo la Dawro kupinduka Jumatano jioni na kusababisha maafa hayo makubwa.

Kwa mujibu wa maafisa wa serikali za kieneo, waliojeruhiwa katika ajali hiyo hivi sasa wanapata matibabu ya kina katika vituo vya afya vya karibu na eneo la ajali hiyo.

Polisi wa Ethiopia nao wamethibitisha habari hiyo na kusisitiza kwamba, kuna uwezekano mkubwa wa kuongozeka idadi ya vifo kutokana na hali mbaya za baadhi ya majeruhi.Mbali na kiwango cha chini cha vyombo vya usafiri, kuna na sababu nyingine mbalimbali ambazo zinazifanya ajali mbaya za barabarani kuwa jambo la kawaida nchini Ethiopia ikiwa ni pamoja na ubovu na hali mbaya za barabara, kuendesha magari bila ya uangalifu, mfumo mbovu wa utoaji wa leseni za udereva, uzembe na kudharau sheria za usafiri wa barabarani.