Wanaorejea Omdurman Sudan waendelea kusakamwa na makombora, njaa na magonjwa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i116824-wanaorejea_omdurman_sudan_waendelea_kusakamwa_na_makombora_njaa_na_magonjwa
Maeneo ya Karari katika mji wa Omdurman wa kaskazini mwa mji mkuu wa Sudan, Khartoum, yamekumbwa na msukosuko mwingine wa mapigano ya uchu wa madaraka baina ya majenerali wa kijeshi wanaoongoza makundi mawili, Vikosi vya wa Msaada wa Haraka (RSF) na Vikosi vya Wanajeshi wa Sudan (SAF).
(last modified 2024-09-27T03:17:29+00:00 )
Sep 27, 2024 03:17 UTC
  • Wanaorejea Omdurman Sudan waendelea kusakamwa na makombora, njaa na magonjwa

Maeneo ya Karari katika mji wa Omdurman wa kaskazini mwa mji mkuu wa Sudan, Khartoum, yamekumbwa na msukosuko mwingine wa mapigano ya uchu wa madaraka baina ya majenerali wa kijeshi wanaoongoza makundi mawili, Vikosi vya wa Msaada wa Haraka (RSF) na Vikosi vya Wanajeshi wa Sudan (SAF).

Hayo ni maeneo ambayo yanajumuisha masoko yenye msongamano mkubwa wa watu na shughuli nyinginezo. Ni maeneo ambayo yana zaidi ya vituo 160 vilivyojaa Wasudan waliokimbia makazi yao kutokana na vita hivyo vya uchu wa madaraka baina ya majenerali wa kijeshi.

Wanaorejea kwenye maeneo hayo hawajawahi kujisikia kuwa na uhakika wa maisha yao, kwani bado wanapigwa ovyo na mizinga tena mara kwa mara. Si hayo tu, lakini pia watu hao wanateseka kwa njaa na magonjwa mbalimbali kutokana na vita kuvuruga mifumo yote ya maisha salama.

Siku ya Jumatatu, takriban watu 15 waliuawa na wengine 61 kujeruhiwa katika shambulio la mizinga la RSF kwenye soko la raia la Sabreen lililokuwa limejaa watu huko Karari.

"Huu ndio ukweli sasa. Tunajaribu kuishi na hali hiyo, lakini tunaogopa kukata tamaa na kukimbia tena," amesema Mahmoud Satti, mwalimu aliyerejea Omdurman baada ya kukimbia na kuishi maeneo ya katikati mwa Sudan kwa muda wa mwaka mzima.

Naye Saeed Al-Zubair mkazi wa Omdurman Sudan mwenye umri wa miaka 49 amesema: "Kuna ongezeko kubwa la magonjwa huku kukiwa na uhaba mkubwa wa dawa, hakuna hospitali za karibu, na hata zile zinazofanya kazi zimeshambuliwa kwa mabomu na kuporwa."