Mkuu wa RSF: Tuko tayari kusitisha vita kuruhusu misaada ya kibinadamu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i116838-mkuu_wa_rsf_tuko_tayari_kusitisha_vita_kuruhusu_misaada_ya_kibinadamu
Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo mkuu wa kikosi cha RSF nchini Sudan, amesema kuwa, kundi hilo liko tayari kutekeleza mpango wa usitishaji vita kote nchini humo ili kuruhusu usambazaji wa misaada ya kibinadamu.
(last modified 2024-09-27T10:08:55+00:00 )
Sep 27, 2024 10:08 UTC
  • Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo
    Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo

Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo mkuu wa kikosi cha RSF nchini Sudan, amesema kuwa, kundi hilo liko tayari kutekeleza mpango wa usitishaji vita kote nchini humo ili kuruhusu usambazaji wa misaada ya kibinadamu.

Kiongozi huyo wa RSF ametoa kauli hiyo baada ya Mkuu wa Jeshi la nchi hiyo Jenerali Abdel-Fattah al-Burhan, kuwatuhumu wanamgambo hao kwamba, wanakwamisha juhudi za amani.

Al-Burhan amelitolea pia wito Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kukitambua Kikosi cha Usaidizi wa Haraka (RSF) kinachoongozwa na hasimu wake Hamdan Dagalo kama kundi la kigaidi, akisema wanaendesha mauaji ya kikabila, kuwalazimisha watu kuyahama makazi yao pamoja na mauaji ya halaiki.

Hayo yanaripotiwa wakati mapigano makali yameendelea kuripotiwa sehemu mbalimbali nchini Sudan ikiwa ni pamoja na mji mkuu Khartoum na mji wa Omdurman.

Idadi ya wakimbizi Sudan imekuwa ikiongezeka kila siku kutokana na vita vinavyoendelea nchini humo

 

Wakati huo huo ripoti zinasema kuwa wapiganaji wa kikosi cha RSF pia wameendelea kusonga mbele katika maeneo mengine ya Sudan katika miezi ya karibuni katika mzozo ambao umesababisha maafa makubwa ya binadamu huko Sudan.

Mapigano ya silaha yalianza huko Sudan Aprili 15 mwaka jana (2023) kati ya jeshi la nchi hiyo (SAF) linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al Burhan ambaye ni kiongozi wa Sudan na wanamgambo wa Kikosi cha Usaidizi wa Haraka (RSF) ambao kamanda wao ni Hamdan Dagalo.

Hadi sasa juhudi za upatanishi wa kimataifa za kuhitimisha mapigano hayo na kuzishawishi pande hasimu kuketi kwenye meza ya mazungumzo zimegonga mwamba.