Afrika kupatiwa zaidi ya dola Mil.800 kukabiliana na Mpox
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i116848-afrika_kupatiwa_zaidi_ya_dola_mil.800_kukabiliana_na_mpox
Imeelezwa kuwa, bara la Afrika litapatiwa zaidi ya dola milioni 800 kwa ajili ya kukabiliana na homa hatari ya Mpox.
(last modified 2024-09-27T22:48:40+00:00 )
Sep 27, 2024 22:48 UTC
  • Afrika kupatiwa zaidi ya dola Mil.800 kukabiliana na Mpox

Imeelezwa kuwa, bara la Afrika litapatiwa zaidi ya dola milioni 800 kwa ajili ya kukabiliana na homa hatari ya Mpox.

Zaidi ya dola milioni 800 ndizo zilizoahidiwa kwa vituo vya kudhibiti na kuzuia magonjwa barani Afrika ili kupambana na mlipuko wa Mpox.

Hayo yameelezwa na Jean Kaseya Mkuu wa Kituo cha Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa Barani Afrika (CDC) ambaye ameongeza kuwa, kiasi hicho ni kikubwa kuliko kiasi kilichotarajiwa cha dola milioni 600.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa takriban kesi 30,000 zinazoshukiwa kuwa za ugonjwa wa Mpox zimeripotiwa mwaka huu barani Afrika, huku wengi wa walioambukizwa wakitoka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Shirika la Afya Duniani limeongeza kuwa, wagonjwa 2,082 walithibitika kuwa na maambukizi ya Mpox duniani kote mwezi Agosti mwaka huu; kiwango ambacho ni cha juu zaidi tangu Novemba mwaka jana.

Chanjo ya homa ya Mpox

Agosti 14 mwaka huu, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitangaza hali ya dharura ya kimataifa kutokana na kusambaa kwa virusi vya mpox, hasa kuongezeka kwa visa vya maambukizi vya aina mpya ya virusi hivyo inayofahamika kama Clade 1b nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Kwa mujibu wa WHO, kanda ya Afrika hivi sasa inashuhudia ongezeko la maambukizo ya homa hiyo, huku mataifa 14 ya bara hilo yakiathirika.

Shirika la Afya Duniani limetangaza kuwa, licha ya kuwa maambukizi ya ugonjwa huo yamekuwa yakiongezeka kwa kasi, lakini vifo vinavyotokana na maradhi hayo ni vichache.