Kassim Majaliwa: Lugha ya Kiswahili iwe lugha rasmi ya 7 ya UN
Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Tanzania amehutubia kwa mara ya kwanza Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani akimwakilisha Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.
Demokrasia, lugha ya Kiswahili, usalama na uhuru wa wananchi, Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs na masuala mengine kama kupigia chepuo uondolewaji wa vikwazo vya uchumi kwa Cuba ni miongoni mwa mambo mengi yaliyopata nafasi katika hotuba ya Majaliwa.
Waziri Mkuu Majaliwa ameeleza namna ambavyo Tanzania imepokea kwa mikono miwili kupitishwa kwa azimio la Baraza Kuu la 78/312, linalotangaza tarehe 7 Julai kuwa Siku ya Kimataifa ya Lugha ya Kiswahili. Kiswahili, lugha inayozungumzwa na zaidi ya watu milioni 200 katika mabara yote ya dunia, ni nyenzo muhimu ya kuendeleza amani, umoja na tofauti za kitamaduni. Ametoa wito kwa Baraza la Usalama kuangalia uwezekano wa kukitambua Kiswahili kuwa lugha rasmi ya 7 ya Umoja wa Mataifa. Kwa sasa lugha rasmi za Umoja wa Mataifa ni 6 ambazo ni Kiarabu, Kichina, Kiingereza, Kifaransa, Kirusi na Kispaniola.
Amesema tayari Muungano wa Afrika, Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika zimeongoza njia kwa kutambua Kiswahili kama lugha rasmi.