Watu 17 wauawa kwa kupigwa risasi kwa umati nchini Afrika Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i116896-watu_17_wauawa_kwa_kupigwa_risasi_kwa_umati_nchini_afrika_kusini
Polisi wa Afrika Kusini wameanzisha msako wa dharura baada ya watu 17 kupigwa risasi na kuuawa kwa umati katika mkoa wa Cape Mashariki.
(last modified 2024-09-29T02:38:40+00:00 )
Sep 29, 2024 02:38 UTC
  • Watu 17 wauawa kwa kupigwa risasi kwa umati nchini Afrika Kusini

Polisi wa Afrika Kusini wameanzisha msako wa dharura baada ya watu 17 kupigwa risasi na kuuawa kwa umati katika mkoa wa Cape Mashariki.

Serikali ya mkoa wa Cape Mashariki imethibitisha katika taarifa yake kwamba "tukio hilo baya" lilitokea jana Jumamosi asubuhi katika mji wa Lusikisiki.

Athlenda Mathe, msemaji wa kitaifa wa Huduma ya Polisi ya Afrika Kusini (SAPS) amesema: "Watu 13 wameuawa katika nyumba moja ambao ni pamoja na wanawake 12 na mwanamume mmoja. Watu wengine wanne wameuawa katika nyumba nyingine."

Pia amesema: "Mhanga wa kumi na nane yuko katika hali mbaya hospitalini. Kwa jumla wanawake 15 na wanaume wawili wameuawa. Polisi tumeanzisha msako mkali ili kuwafikisha wale waliohusika na mauaji haya ya kikatili mbele ya sheria. Tumejitolea kuhakikisha usalama na amani inadumishwa ndani ya jamii zetu."

Katika taarifa ya serikali ya mkoa, Waziri Mkuu wa Cape Mashariki, Oscar Mabuyane amelaani jinai hiyo kwa kutumia maneno makali sana. 

"Kupoteza maisha kwa kiwango hiki ni pigo kubwa kwa jimbo letu, na tunaomboleza vifo cha watu hawa wasio na hatia. Tuko pamoja na familia na jamii zilizoathirika. Mauaji ya kikatili na ya kinyama ya watu wasio na hatia ni kitendo cha kutisha ambacho hakina nafasi katika jamii yetu,” alisema Mabuyane.

Vile vile amesisitiza kuwa: "Tunatoa wito kwa wakazi wote wa Cape Mashariki kusimama pamoja katika kukemea ghasia na kushirikiana katika kujenga jimbo salama na lenye amani zaidi."