Sheikh Zakzaki: Kicheko cha adui Mzayuni hakitodumu muda mrefu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i116996-sheikh_zakzaki_kicheko_cha_adui_mzayuni_hakitodumu_muda_mrefu
Sheikh Ibrahim Zakzaki, Mkuu wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria amegusia jinsi utawala wa Kizayuni ulivyomuua kigaidi Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon na kusema kuwa, maadui wamefanya sherehe kufuatia jinai hiyo ya kigaidi kama walivyofanya sherehe waliomuua Imam Husain AS huko Karbala, lakini vicheko vyao havitodumu muda mrefu.
(last modified 2024-10-01T22:48:30+00:00 )
Oct 01, 2024 22:48 UTC
  • Sheikh Ibrahim Zakzaki
    Sheikh Ibrahim Zakzaki

Sheikh Ibrahim Zakzaki, Mkuu wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria amegusia jinsi utawala wa Kizayuni ulivyomuua kigaidi Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon na kusema kuwa, maadui wamefanya sherehe kufuatia jinai hiyo ya kigaidi kama walivyofanya sherehe waliomuua Imam Husain AS huko Karbala, lakini vicheko vyao havitodumu muda mrefu.

Amesema kuwa, istihzai za maadui hazimuongezei muumini isipokuwa thawabu na kwamba kama walivyofanya wafuasi wa Yazid ambao walisherehekea mauaji ya mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW) Imam Husain (AS) huko Karbala mwaka 61 Hijria lakini leo jina la Husain na mapambano yake linameremeta kila kona, ni vivyo hivyo vicheko vya maadui wa hivi sasa pia havitodumu. 

Ameongeza kuwa, roho ya Sayyid Hassan Nasrullah iko hai na itaendelea kuwaandama maadui popote wanapojificha. Amesema: Roho tukufu ya Sayyid Hassan Nasrullah itapelekea kushuhudiwa ushindi mkubwa dhidi ya Wazayuni karibuni hivi.

Wakati huo huo Mahmoud Qatati, mjumbe wa Baraza la Kisiasa la Harakati ya Hizbullah ya Lebanon jana Jumanne alisisitiza kuwa wanajeshi wa utawala wa Kizayuni hawajathubutu kuingia hata kwa sentimita moja ndani ya ardhi ya Lebanon.

Vilevile amesema kuwa ushahidi wa nguvu za Hizbullah ni jinsi harakati hiyo ya Kiislamu ilivyopiga umbali wa kilomita 150 ndani ya ardhi za Palestina zilizopachikwa jina bandia la Israel na kusisitiza kuwa, harakati hiyo ya Muqawama wa Kiislamu iko tayari kwa lolote lile.

Afisa huyo wa Hizbullah ya Lebanon vilevile amesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni muungaji mkono mkuu wa kambi ya Muqawama na itaendelea kuwa hivyo daima akisisitiza kwamba si jambo linaloingia akilini kudhani kwamba katika mazingira kama ya sasa, Iran itaachana na kambi ya Muqawama.