Boti 2 za wahamiaji zimezama katika Bahari Nyekundu kwenye pwani ya Djibouti na kuua 45
(last modified Thu, 03 Oct 2024 08:01:23 GMT )
Oct 03, 2024 08:01 UTC
  • Boti 2 za wahamiaji zimezama katika Bahari Nyekundu kwenye pwani ya Djibouti na kuua 45

Boti mbili zilizokuwa zimebeba wahamiaji wa Kifrika zimezama katika Bahari Nyekundu kwenye pwani ya Djibouti, na kuua watu 45. Hayo ni kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Uhamiaji la Umoja wa Mataifa (IOM).

"Boti hizo zilianza safari zao kuotoka Yemen zikiwa zimebeba watu 310", limesema Shirika  la Kimataifa la Uhamiaji.

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa, ambalo limekuwa likisaidia juhudi za utafutaji na uokoaji wahamiaji, limesema kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba manusura 32 wameokolewa.

Wahamiaji wakiwa baharini

Kikosi cha Ulinzi wa Pwani cha Djibouti kimesema mkasa huo ulitokea umbali wa mita 150 (kama futi 500) kutoka ufuo wa bahari karibu na eneo la kaskazini magharibi la Khor Angar. Kimesema juhudi za pamoja za uokoaji zinaendelea na kwamba manusura 115 wameokolewa.

Maelfu ya wahamiaji kutoka nchi za Afrika, Mashariki ya Kati na Kusini mwa Asia wamekuwa wakijaribu kuvuka maji ya bahari na kuelekea Ulaya kwa lengo la eti kutafuta maisha bora barani.

Magenge ya wasafirishaji haramu hupakia meli zilizojaa watu ambao huwa tayari kuhatarisha maisha yao ili kufika bara la Ulaya.