Hasira zatanda Afrika Kusini baada ya wakulima wazungu kuwaua wazalendo na kuwafanya chakula cha nguruwe
Gazeti la New York Times limeripoti kwamba, habari ya kutisha inayosema wakulima weupe waliwaua wanawake wawili na kuwalisha nguruwe maiti zao imezua mjadala kuhusu baadhi ya masuala tata zaidi nchini Afrika Kusini, kama vile ubaguzi wa rangi, unyanyasaji kwa msingi wa nafasi ya kijamii na umiliki wa mashamba.
Ripoti iliyoandikwa na mkuu wa ofisi ya gazeti hilo la Marekani mjini Johannesburg, John Eligon, imesema kwamba, wanawake wawili weusi walioingia katika shamba linalomilikiwa na wazungu kwa ajili ya kufatuta chakula kinachotupwa jalalani wiki kadhaa zilizopita, hawakurudi kamwe.
Mmiliki wa shamba hilo na wafanyakazi wake wawili wanatuhumiwa kuwa waliwapiga risasi na kuwaua wanawake hao wawili na kisha kutupa miili yao kwenye zizi la nguruwe, ambapo polisi wanasema wamepata miili hiyo ikiwa imeoza na kuliwa kiasi na nguruwe hao.
Tukio hili limezua hasira katika jimbo la Limpopo kaskazini mashariki mwa Johannesburg na kuibua mjadala juu ya masuala kadhaa nchini Afrika Kusini, kama vile rangi na mbari za watu, ukatili unaojiegemeza kwenye hadhi na nafasi ya kijamii na umiliki wa ardhi kati ya wakulima wazungu na majirani zao, wazalendo weusi.
Wanawake wawili waliouawa na maiti zao kuliwa na nguruwe, Maria Makgatho (umri wa miaka 44) na Lokadia Ndlovu (umri wa miaka 35), waliingia shambani wakitafuta chakula katikati ya mwezi Agosti baada ya lori la kampuni ya maziwa kutupa bidhaa zilizokwisha muda wake. Mume wa Makgatho alipigwa risasi, lakini alinusurika na kukimbia.
Wazalendo weusi wameandamana nje ya mahakama, huku wanasiasa wakitoa kauli za hasira, na wengine wakisema kwamba tukio hilo linakumbusha suala pana la kutokuwepo usawa katika umiliki wa ardhi nchini Afrika Kusini, tangu utawala wa ubaguzi wa rangi ulipowalazimisha weusi wengi kutoka kwenye ardhi na mashamba yao.

Leo hii, mashamba mengi makubwa ya kibiashara nchini Afrika Kusini yanasalia chini ya umiliki wa wazungu, huku watu weusi katika maeneo ya vijijini wakiendelea kuishi katika umaskini, na kutafuta chakula kilichoisha muda wake kwenye mashamba ya wazungu.