Gachagua mashakani, Bunge la Kenya kumsaili Naibu Rais leo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i117254-gachagua_mashakani_bunge_la_kenya_kumsaili_naibu_rais_leo
Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua, leo atafahamu iwapo atanusurika au kupoteza nafasi hiyo, wakati mchakato wa kuvuliwa wadhifa wake utakapoanza  huku wabunge wakitarajiwa kupigia kura hoja ya kutokuwa na imani na uongozi wake.
(last modified 2024-10-08T01:12:07+00:00 )
Oct 08, 2024 01:12 UTC
  • Rigathi Gachagua
    Rigathi Gachagua

Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua, leo atafahamu iwapo atanusurika au kupoteza nafasi hiyo, wakati mchakato wa kuvuliwa wadhifa wake utakapoanza  huku wabunge wakitarajiwa kupigia kura hoja ya kutokuwa na imani na uongozi wake.

Bunge la Kitaifa asubuhi hii litaanza kwa kujadili hoja ya kumng’oa madarakani Bw Gachagua ambayo iliwasilishwa wiki jana na mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse.

Hoja hiyo ilitiwa saini na wabunge 291 na iwapo itaungwa mkono na theluthi mbili ya wabunge 233 kati 349 basi itapelekwa kwenye Bunge la Seneti ndani ya siku mbili.

Hata hivyo, Bw Gachagua anaweza kunusurika tu iwapo wabunge 117  watapiga kura ya kupinga hoja hiyo.

Wikendi, Bw Gachagua akionekana mnyonge na mnyekekevu alishiriki ibada ambayo huenda ilikuwa ya mwisho katika makazi ya Naibu Rais kama wabunge watamtimua leo na seneti kuhalalisha hilo mnamo Alhamisi.

Wakati wa ibada hiyo mbunge huyo wa zamani wa Mathira alimwomba msamaha Rais William Ruto na wabunge, akisema ana majuto iwapo walikwaruzana wakati wa kuwahudumia Wakenya.

Mbele ya Bunge leo Jumanne, Naibu Rais atakuwa na mlima wa kuukwea katika mashtaka 11 ambayo yaliwasilishwa dhidi yake na Bw Mutuse wiki jana.

Ili kungátuliwa kwake, bunge linahitaji kudhibitisha tu kuwa kuna ushahidi wa kutosha kwenye shtaka moja na kulipitisha shtaka hilo.