Watu 7 wameuawa, 59 wajeruhiwa katika shambulizi la makombora Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i117256-watu_7_wameuawa_59_wajeruhiwa_katika_shambulizi_la_makombora_sudan
Takriban watu saba wameuawa na wengine 59 wamejeruhiwa katika shambulio lililofanywa na Vikosi vya Msaada wa Hharakati (RSF) kwenye kambi ya wakimbizi huko El Fasher, Darfur Kaskazini nchini Sudan.
(last modified 2024-10-08T02:19:21+00:00 )
Oct 08, 2024 02:19 UTC
  • Watu 7 wameuawa, 59 wajeruhiwa katika shambulizi la makombora Sudan

Takriban watu saba wameuawa na wengine 59 wamejeruhiwa katika shambulio lililofanywa na Vikosi vya Msaada wa Hharakati (RSF) kwenye kambi ya wakimbizi huko El Fasher, Darfur Kaskazini nchini Sudan.

Ibrahim Khatir, Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya ya Darfur Kaskazini ametangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, shambulio hilo limefanywa dhidi ya kambi ya Abu Shouk na liliendelea kwa muda wa siku mbili. Watu wawili waliuawa juzi Jumapili na wengine watano waliuawa jana Jumatatu. Mkurugenzi huyo wa Wizara ya Afya ya Darfur Kaskazini nchini Sudan ameongeza kuwa, watu 20 walijeruhiwa katika shambulio la siku ya Jumapili na wengine 39 walijeruhiwa jana Jumatatu.

Kwa upande wake, Mtandao wa Madaktari wa Sudan; ambalo ni shirika lisilo la kiserikali, umelaani mashambulizi ya makombora katika maeneo ya raia na kusema kuwa, mashambulio hayo yanazidisha mateso kwa watu waliokimbia makazi yao ambao tayari wanateseka kwa hali mbaya iliyoambatana na kuendelea vita visivyo na mwisho nchini humo.

Raia wa kawaida ndio wahanga wakuu wa vita vya uchu wa madaraka baina ya majenerali wa kijeshi Sudan

 

Mapigano ya uchu wa madaraka baina ya majenerali wa kijeshi wanaoongoza makundi mawili yaani Jeshi la Sudan (SAF) na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) yamepamba moto huko El Fasher tangu Mei 10. Mji huo, una kambi tatu za wakimbizi. Moja ya kambi hizo ni Abu Shouk ambayo ina karibu wakimbizi milioni 1.5. Laki nane kati ya wakimbizi hao ni wakimbizi wa ndani. Hayo ni kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa.

Sudan imekumbwa na mgogoro mkubwa kati ya SAF na RSF tangu Aprili 15, 2023. Takriban watu 20,000 wameshauawa na mamilioni ya wengine wamekuwa wakimbizi ndani na nje ya Sudan.