Oct 08, 2024 12:45 UTC
  • Burkina Faso yasimamisha matangazo ya VOA ya Marekani

Serikali ya Burkina Faso imesimamisha matangazo ya shirika la utangazaji la Sauti ya Marekani (VOA) linalofadhiliwa na Washington kwa muda wa miezi mitatu kwa 'kushajiisha ugaidi.'

Baraza Kuu la Mawasiliano nchini humo (CSC) limeishutumu VOA kwa kuwakatisha tamaa wanajeshi wa nchi hiyo ya Afrika Magharibi na nchi jirani ya Mali, wakati wa kipindi cha mjadala kilichorushwa hewani Septemba 19, ambacho pia kilitangazwa na kituo binafsi cha redio.

Limesema, kwenye mjadala huo, mwandishi wa habari wa VOA alilielezea shambulio la kigaidi katika mji wa Bamako mwezi uliopita kuwa wa "kijasiri", huku akikosoa operesheni za maafisa usalama, na vile vile kutoa idadi isiyo sahihi ya vifo kwenye shambulio hilo ambalo liliua mamia ya watu mwezi Agosti.

Baraza Kuu la Mawasiliano la Burkina Faso limesisitiza kuwa, wakati wa mjadala huo, ukiukwaji kadhaa wa vifungu vya sheria ulibainika.

Serikali ya kijeshi ya Burkinabe ilipopiga marufuku BBC na VOA

Aprili mwaka huu pia, Burkina Faso ilisimamisha matangazo ya shirika la utangazaji la BBC ya Uingereza na VOA ya Marekani, kwa kuripoti uchunguzi wa Human Rights Watch ambao ulidai kwamba jeshi la Burkina Faso liliwanyonga wanakijiji wapatao 223 mwezi Februari, eti kama sehemu ya operesheni yake dhidi ya raia wanaotuhumiwa kushirikiana na wanamgambo wa kigaidi.

Kadhalika serikali za Niger na Burkina Faso zimewahi huko nyuma kusimamisha nchini humo matangazo ya redio ya Kifaransa ya RFI na televisheni ya France 24 zinazofadhiliwa na serikali ya Paris, kwa madai ya kutangaza habari za uwongo na upotoshaji.

Tags