Seneti ya Kenya kusikiliza hoja ya kumtimua Naibu Rais, Gachagua
-
Amason Kingi
Spika wa Seneti ya Kenya, Amason Kingi, ameagiza kikao cha Baraza la Seneti kusikiza hoja ya kumtimua Naibu Rais Jumatano na Alhamisi wiki ijayo.
Hii ni baada ya Seneta wa Nairobi, Edwin Sifuna, kukosa kuunga mkono pendekezo la Kiongozi wa Wengi katika Seneti, Aaron Cheruiyot la kubuniwa Kamati Maalumu ya maseneta 11 kusikiza hoja ya kumtimua Gachagua.
Baraza la Seneti ya Kenya sasa litakuwa na muda wa siku mbili kusikiza mashtaka 11 yaliyowasilishwa dhidi ya Naibu Rais wa nchi hiyo, Rigathi Gachagua.

Spika Seneti Amason Kingi amesema Seneti itahakikisha kila upande umepata muda wa kutosha kujitetea na kuwasilisha upande wake.
Itakumbukwa kuwa, Bunge la Kitaifa la Kenya jana Jumanne lilipasisha kwa wingi wa kura hoja ya kumng’oa madarakani Naibu Rais wa nchi hiyo, Rigathi Gachagua.
Mbunge wa Kibwezi Magharibi, Mwengi Mutuse aliwasilisha mashtaka 11 yaliyojumuisha ulimbikizaji wa mali ya Shilingi bilioni 5.2 za Kenya kupitia njia za ufisadi katika miaka miwili akiwa naibu rais pamoja na madai ya kuwagawanya Wakenya kwa kauli yake kwamba serikali ya Kenya Kwanza imeundwa na ‘wenye hisa’ pekee.