Umoja wa Mataifa: Visa vya kipindupindu vyaongezeka Sudan
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, visa vya ugonjwa wa kipindupindu vimeongezeka nchini Sudan kwa karibu asilimia 40 chini ya kipindi cha wiki mbili.
Takwimu hizo za hivi karibuni zimeibua wasiwasi kwa maafisa wa afya wa Umoja wa Mataifa ambao kwa muda mrefu wameonya kuhusu mripuko huo, na kukosekana kwa njia sahihi za kupambana nao tangu uliporipotiwa mwezi Julai mwaka huu.
Wizara ya Afya ya Sudan imesema katika taarifa yake kuwa, karibu visa 21,288 viliripotiwa kwenye majimbo 11 kati ya 18 katika kipindi hicho pamoja na vifo 626.
Visa vingi vya maambukizi vilikuwa katika mji wa Kassala ambako Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia Watoto, UNICEF linashirikiana na wizara ya afya na Shirika la Afya Duniani, WHO katika kutoa awamu ya pili ya chanjo ya matone ya kipindupindu iliyoanza mwezi uliopita.
Mwishoni mwa mwezi Agosti, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR lilitangaza kupitia mwakilishi wake nchini Sudan, Kristine Hambrouck kwamba mripuko mpya wa kipindupindu nchini humo ambao ni wimbi la pili tangu vilipoanza vita vya uchu wa madaraka baina ya majenerali wa kijeshi.
Imeelezwa pia kuwa, mapigano, kukosekana usalama na mvua zinazoendelea kunyesha vinatatiza usafirishaji wa misaada ya kibinadamu. Katika majimbo ya Sennar, Blue Nile, Jazirah, White Nile, Darfur na Kordofan - yanayotoa hifadhi kwa zaidi ya wakimbizi milioni saba na laki nne pamoja na wakimbizi wa ndani wa Sudan - kuna changamoto za upatikanaji wa huduma kwa kuchelewesha utoaji wa dawa muhimu na vifaa vya msaada.