Umoja wa Mataifa: Watu milioni moja wamehama makazi yao DRC
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, kwa akali watu milioni moja wamehama makazi yao katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kufuatia kuzorota hali ya usalama katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.
Hayo yameelezwa na Volker Turk Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu ambaye amebainisha kuwa, hali ya haki za binadamu inaendelea kuwa mbaya mbele ya macho yetu".
Akizungumza mbele ya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa Volker Türk amesema: Mchanganyiko wa kuongezeka kwa ghasia, maslahi ya kikanda na kimataifa, uchimbaji haramu wa madini na utawala dhaifu wa sheria kwa madhara ya watu ambao tayari wameharibiwa na miongo kadhaa ya migogoro, ni miongoni mwa mambo ambayo yamezidi kuzotoshea amani na kuheshimiwa haki za binadamu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Aidha amesema, Kati ya Juni 1, 2023 na Mei 31, 2024, asilimia 85 ya visa vya ukiukaji na mashambulizi yaliyofanywa nchini DRC yalifanyika katika mikoa iliyoathiriwa na vita mashariki mwa nchi. Wapiganaji wa makundi yenye silaha wanaaminika kuhusika na 61% ya vitendo hivyo, pamoja na mashambulizi mabaya dhidi ya raia na miundombinu ya kiraia, ikiwa ni pamoja na shule na hospitali.
Unyanyasaji wa kijinsia unaenea, huku waathiriwa wapya 700 wakitambuliwa. "Makundi yenye silaha huteka nyara, kushikilia mateka na kuwaweka wanawake na wasichana katika utumwa wa ngono, wengi wao wameuawa baada ya kubakwa," Türk amesema.