Kenya yawa mwanachama wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa la
(last modified Thu, 10 Oct 2024 11:13:32 GMT )
Oct 10, 2024 11:13 UTC
  • Kenya yawa mwanachama wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa la

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limeichagua Kenya kuwa mwanachama katika Baraza la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu, kuanzia Januari mwakani (2025).

Kenya ilichaguliwa pamoja na mataifa mengine 18 ambayo ni Benin, Bolivia, Colombia, Cyprus, Czechia, Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Ethiopia, Gambia, Iceland, Marshall Islands, Mexico, North Macedonia, Qatar, Jamuhuri Korea, Uhispania, Switzerland na Thailand.

Umoja wa Mataifa umesema katika taarifa yake kwamba, mataifa hayo yatahudumu kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia Januari Mosi, 2025.

Kenya ilituma ombi kuwa mwanachama wa baraza hilo Septemba 27,2024.

Nchi hizo zilizochaguliwa zinatarajiwa kudhihirisha viwango vya juu vya kutetea haki za kibinadamu, ikiwa ni pamoja na kutekeleza kikamilifu mifumo ya Umoja wa Mataifa.

Hata hivyo Tume ya kutetea haki za binadamu nchini Kenya ilikuwa imeliandikia barua baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa kupinga ombi la Kenya la kutaka kujiunga na baraza hilo.

Akizungumza katika kikao na wanahabari, naibu mkurugenzi mtendaji wa tume ya kutetea haki za binadamu nchini Cornelius Oduor alilalamika kuwa Kenya haistahili kuwa katika baraza hilo akitoa mfano wa ukiukaji wa haki za binadamu.

Makundi ya kutetea haki za binadamu nchini Kenya yanapinga Kenya kupewa fursa hiyo kwa madai kwamba serikali iliyopo madarakani “imehusika na ukiukaji wa haki za kibinadamu”.

Aidha yamenukuu ukiukwaji wa haki za binadamu kama vile mauaji ya kiholela, utekaji nyara na kutoweka kwa raia wakiwa mikononi mwa polisi.