Kongo yawazika kwa umati wahanga wa ajali mbaya ya boti
(last modified Fri, 11 Oct 2024 02:38:08 GMT )
Oct 11, 2024 02:38 UTC
  • Kongo yawazika kwa umati wahanga wa ajali mbaya ya boti

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imewazika kwa umati watu waliopatikana katika ajali mbaya ya boti iliyosababisha vifo vya watu 78 kwenye Ziwa Tanganyika. Maziko hayo yamefanyika katika mkoa wa Kivu Kaskazini.

Taarifa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zinasema kuwa, watu hao wamezikwa katika makaburi ya Nyirangongo na shughuli hiyo imehudhuriwa na umati mkubwa wa watu wenye majonzi pamoja na viongozi kutoka sekta mbalimbali na wawakilishi wa makundi ya kiraia wakiongozwa na mawaziri wa mambo ya ndani na masuala ya kijamii wa DRC.

Familia za watu hao bado zimo kwenye majonzi makubwali huku wengi wao wakiwa hawajui jamaa zao wako wapi. Serikali ya DRC imesema kuwa, juhudi za kutafuta watu zaidi zinaendelea, lakini pia imeziambia familia hizo kwamba uwezekano wa kuwapata watu wakiwa hai ni mdogo. 

Majonzi na huzuni imefunika mashariki mwa DRC

 

Baadhi ya watu wa familia wamelalamikia kile wanachokiona kuwa ni maamuzi ya upande mmoja ya serikali na kusema kuwa inapuuza uchungu wa familia ambazo hadi hivi sasa hazijui hatima ya wapendwa wao. Watu wengine wameamua kumwachia Mungu lakini wengine wana matumaini ya kuwapata jamaa zao kutokana na juhudi zinazoendelea za kutafuta watu zaidi. 

Hatua za kisheria zinatarajiwa kuchukuliwa dhidi ya kila aliyefanya uzembe na aliyesababisha ajali hiyo mbaya ya boti ya MV Merdi iliyotokea siku ya Alkhamisi. Wingu la huzuni limeendelea kutanda katika majimbo mawili ya Kivu Kaskazini na Kusini, mashariki mwa DRC. 

Ajali za boti ni kitu cha kawaida nchini Kongo. Rushwa, kwenda mwendo wa kasi na kujaza abiria na mizigo kupindukia ni miongoni mwa sababu kuu za wingi wa ajali hizo.