UN na Sudan Kusini zatia saini makubaliano ya kukabiliana na mafuriko
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i117400-un_na_sudan_kusini_zatia_saini_makubaliano_ya_kukabiliana_na_mafuriko
Sudan Kusini na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Inayohusiana na Miradi (UNOPS) jana Ijumaa zilitiliana saini makubaliano ya kununua vifaa muhimu vya kukabiliana na mafuriko kwa ajili ya kaunti zilizokumbwa na mafuriko Sudan Kusini huku idadi ya watu walioathiriwa na mafuriko hayo ikiongezeka hadi 893,000.
(last modified 2024-10-11T23:19:11+00:00 )
Oct 11, 2024 23:19 UTC
  • UN na Sudan Kusini zatia saini makubaliano ya kukabiliana na mafuriko

Sudan Kusini na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Inayohusiana na Miradi (UNOPS) jana Ijumaa zilitiliana saini makubaliano ya kununua vifaa muhimu vya kukabiliana na mafuriko kwa ajili ya kaunti zilizokumbwa na mafuriko Sudan Kusini huku idadi ya watu walioathiriwa na mafuriko hayo ikiongezeka hadi 893,000.

Mkataba huo wenye thamani ya dola 299,000 umetiwa saini na Wizara ya Rasilimali za Maji na Umwagiliaji ya Sudan Kusini na ofisi hiyo ya Umoja wa Mataifa na unatarajiwa kuongeza vifaa vya kukabiliana na mafuriko kwa ajili ya kaunti za Bor na Fangak za majimbo ya Jonglei na Pibor.

Peter Malual Dhieu Akat, katibu mkuu wa wizara hiyo amethibitisha taarifa hiyo na kusema baada ya kusaini mkataba huo huko Juba, mji mkuu wa Sudan Kusini kwamba: "Tunaiomba UNOPS kuharakisha hatua za kukabiliana na mafuriko ambayo tayari yameharibu mashamba na kushughulikia hali hii ya sasa ambayo inaathiri watu wetu na inaongeza ugumu ambao watu wetu wengi wanakabiliana nao."

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa mvua imewakosesha makazi watu 241,000 katika kaunti 16 za Sudan Kusini

 

Makubaliano hayo, ambayo yataendelea hadi mwezi Februari 2025, ni sehemu ya Mradi wa Kikanda wa Kukabiliana na Majanga ya Tabianchi unaofadhiliwa na Benki ya Dunia kwa ajili ya nchi za mashariki na kusini mwa Afrika. UNOPS itasimamia ununuzi na usambazaji wa vifaa vya kukabiliana na mafuriko kwa kushirikiana na wizara hiyo na serikali za mitaa za Sudan Kusini.

Makubaliano hayo yamekuja baada ya zoezi la kufikisha misaada ya kibinadamu Sudan Kusini kuwa zito kutokana na mafuriko na mvua inayozidi kunyesha, ambapo kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa mvua imeshawakosesha makazi watu 241,000 katika kaunti 16 za nchi hiyo.