Misri, Somalia na Eritrea zaunda muungano kukabiliana na Ethiopia
Marais wa Somalia, Eritrea, na Misri wamekubaliana kuongeza ushirikiano kwa ajili ya usalama wa kikanda huku kukiwa na mvutano baina ya nchi hizo tatu na Ethiopia.
Mkutano huo wa pande tatu, uliofanyika katika mji mkuu wa Eritrea, Asmara, siku ya Alhamisi, uliitishwa na Rais wa Eritrea Isaias Afwerki na kujumuisha mwenzake wa Misri Abdel Fattah al-Sisi na Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia.
Katika taarifa iliyotolewa na wizara ya habari ya Eritrea, viongozi hao watatu walikubaliana kuimarisha uhusiano na kuboresha uthabiti wa kikanda, na kuheshimiwa mamlaka ya kujitawala na mipaka ya nchi za eneo.
Viongozi hao pia walisisitiza umuhimu wa “kukabiliana na kuingiliwa kwa masuala ya ndani ya nchi za eneo hilo kwa kisingizio chochote; kuratibu juhudi za pamoja za kufikia utulivu wa kikanda na kuunda hali inayofaa kwa ajili ya maendeleo ya pamoja na endelevu”.
Makubaliano hayo ya usalama yanaweza kushadidisha taharuki baina ya nchi hizo na Ethiopia, ambayo ina maelfu ya wanajeshi katika nchi jirani ya Somalia inayopambana na makundi ya kigaidi. Ethiopia imetia saini mapatano ya kutumia bandari ya eneo la Somaliland ambalo limejitangazia uhuru kutoka Somalia. Serikali ya Somalia imepinga vikali mapatano hayo. Eritrea nayo imekuwa na mvutano na Ethiopia kuhusu utumizi wa bandari katika Bahari ya Sham. Misri ambayo inapinga hatua ya Ethiopia kujenga bwawa katika Mto Nile sasa imeungana na Somalia na Eritrea katika kukabiliana na Ethiopia.