Kenya kupeleka kikosi kingine cha polisi nchini Haiti
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i117410-kenya_kupeleka_kikosi_kingine_cha_polisi_nchini_haiti
Rais William Ruto wa Kenya amesema nchi yake itapeleka kikosi kingine cha maafisa 600 wa polisi nchini Haiti ili kusaidia juhudi za kudumisha amani nchini humo.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Oct 12, 2024 03:50 UTC
  • Kenya kupeleka kikosi kingine cha polisi nchini Haiti

Rais William Ruto wa Kenya amesema nchi yake itapeleka kikosi kingine cha maafisa 600 wa polisi nchini Haiti ili kusaidia juhudi za kudumisha amani nchini humo.

Rais Ruto amesema hayo katika mkutano wake na waandishi wa habari katika ikulu ya Nairobi akiwa mwenyeji wa Waziri Mkuu wa Haiti Garry Conille, na kueleza kwamba, bajeti ambayo taifa hilo inayo itakidhi mahitaji ya kikosi kilichoko Haiti hadi mwezi Machi mwaka ujao.

Rais William Ruto ambaye amekuwa akipigia debe amani katika taifa hilo la Carribean amesema kuwa, tangu vikosi vya polisi vya Kenya vitue katika nchi hiyo ambayo imeathiriwa na magenge ya wahalifu, mwanga wa matumiani wa amani umeanza kuonekana hatua ambayo imeanza kurejesha imani ya raia wa Haiti.

 

Rais wa Jamhuri ya Kenya ameeleza kuwa, kwa sasa kikosi cha maafisa 600 wa polisi  wa nchi hiyo kinachotarajiwa kuelekea katika taifa la hilo kinafanya mafunzo kabla ya kuondoka.

Ruto amesema kuwa maafisa wa Kenya wanashirikiana na wenzao wa Haiti kulinda miundombinu na kujenga mazingira bora ya kuishi.

Rais Ruto amesema hadi kufikia sasa shule kadhaa zimefunguliwa, uwanja wa ndege pamoja na hospitali kwenye himaya za makundi ya kihalifu.

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Haiti, Garry Conille ameyataka mataifa wafadhili kutoa rasilimali zaidi ili kuhakikisha kuwa taifa hilo linakuwa thabiti.

Alibainisha kuwa uamuzi wa Umoja wa Mataifa wa kuongeza muda wa vikosi vya kudumisha usalama nchini humo kwa mwaka mmoja unaashiria msaada mkubwa kutoka kwa jamii ya kimataifa.