Rais wa Cameroon atoweka hajulikani alipo
Kutoonekana hadharani kwa Rais Paul Biya wa Cameroon mwenye umri wa miaka 91 kwa siku 30 zilizopita kumeisukuma nchi hiyo ya Afrika ya Kati katika hali ya kutokuwa na uhakika na uvumi kuhusiana na hali yake.
Tangu mwanzoni mwa mwezi Septemba, rais wa Cameroon ametoweka, na hivyo kuchochea uvumi kuhusu afya ya mzee huyo wa miaka 91 na hata kwamba huenda amekufa.
Rais Paul Biya, mwenye umri wa miaka 91, aliye madarakani tangu mwaka 1982, alitarajiwa awe amefika New York mwezi uliopita kushiriki vikao vya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) lakini alishindwa kujitokeza, na vile vile hakutokea kabisa katika mkutano wa kilele wa nchi za Francophone nchini Ufaransa.
Nchini Cameroon, mambo mawili haya muhimu yamezua uvumi kuhusu afya ya Paul Biya na mahali alipo. Serikali siku ya Jumanne iliyopita ilisema kuwa, yuko katika hali nzuri kiafya lakini pamoja na hayo haikutoa maelezo zaidi kuhusiana na suala hilo.