Gavana, mbunge wakamatwa Kenya baada ya mapigano ya koo kuua watu 18
Gavana wa eneo la Tana River Kenya Dhado Godhana alikamatwa Jumamosi jioni kufuatia mapigano makali baina ya koo hasimu ambayo yamesababisha vifo vya watu 18 katika kipindi cha wiki iliyopita.
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) nchini Kenya Mohamed Ibrahim Amin amewathibitishia waandishia wa habari kuwa Godhana na Mbunge wa Galole, Hiribae Said Buya, wamekamatwa baada ya kukataa kufika katika idara ya polisi kujibu maswali kuhusu uwezekano wao wa kuhusishwa na mapigano yanayoendelea.
Mwenyekiti wa Baraza la Magavana wa Kenya (CoG) Ahmed Abdullahi amelaani kukamatwa kwa Godhana, akisema alivunjiwa heshima wakati wa kutiwa mbaroni.
Mapigano hayo, yaliyoanza wiki jana, yameua watu 14 kufikia mapema Jumamosi, hata hivyo, Kamishna wa Kaunti ya Tana River David Koskei amethibitisha kwamba watu wanne zaidi waliuawa Jumamosi, na kufanya jumla ya watu kufikia 18.
Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki, katika notisi ya Gazeti la Serikali, ametangaza baadhi ya maeneo ya Kaunti ya Tana River kuwa yenye matatizo ya usalama na hatari ili kuwezesha vikosi vya usalama kuchukua hatua maalumu za kurejesha utulivu.