Maalim Seif kuishitaki serikali ya Zanzibar ICC hii leo
Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad anatazamiwa kuwasilisha mashtaka dhidi ya serikali ya Zanzibar hii leo mbele ya Mahakama ya Uhalifu ya Kimataifa (ICC).
Kwa mujibu wa duru za kuaminika, Maalim Seif anakwenda ICC kuwashtaki viongozi wa serikali ya sasa visiwani humo chini ya chama tawala CCM, kwa kutumia mamlaka yao vibaya wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka jana katika kuwatesa, kuwakamata na kuwapiga wafuasi wa chama chake cha CUF bila makosa. Hayo yanajiri katika hali ambayo polisi ya Tanzania inasubiri faili la mashtaka dhidi ya Maalim Seif kutoka kwa Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP), ili imburuze mahakamani mwanasiasa huyo.
Itakumbukwa kuwa, tarehe 22 Mei mwaka huu, chama hicho kilizindua ripoti yake inayohusiana na uvunjwaji wa haki za binadamu visiwani Zanzibar wakati wa kujiri uchaguzi huo wa tarehe 25 Oktoba mwaka jana, huku kikitangaza azma yake ya kwenda mahakama hiyo ya ICC kwa lengo la kuwashtaki Waziri wa Mambo ya Ndani na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP). Naibu Katibu Mkuu wa chama cha wananchi CUF Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui amenukuliwa akisema kuwa tayari mpango huo umekamilika na Maalim Seif ambaye yupo nje ya nchi kwa ziara ya kuelezea kile kilichojiri katika uchaguzi mkuu uliopita, ataweka wazi kila kitu kilichotokea na jinsi ukiukwaji demokrasia ulivyoshika kasi nchini Tanzania.