Maambukizi ya Ebola DRC yafikia 710 huku hofu ikitanda
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i139130-maambukizi_ya_ebola_drc_yafikia_710_huku_hofu_ikitanda
Idadi ya visa vilivyothibitishwa vya Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) imefikia 710, wakiwemo watu 149 waliofariki dunia, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Jumamosi na Wizara ya Afya ya nchi hiyo.
(last modified 2026-06-14T11:58:50+00:00 )
Jun 14, 2026 11:57 UTC
  • Maambukizi ya Ebola DRC yafikia 710 huku hofu ikitanda

Idadi ya visa vilivyothibitishwa vya Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) imefikia 710, wakiwemo watu 149 waliofariki dunia, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Jumamosi na Wizara ya Afya ya nchi hiyo.

Hata hivyo, mamlaka zimekanusha uvumi uliosambaa mitandaoni ukidai kuwa serikali imeweka amri ya kufungwa shughuli zote (lockdown) kutokana na mlipuko huo.

Kwa mujibu wa takwimu za wizara, kiwango cha vifo miongoni mwa walioambukizwa  ni asilimia 21.0. Jumla ya wagonjwa 324 wapo katika vituo vya kutengwa au wamelazwa hospitalini, huku watu 35 wakiripotiwa kupona.

Wizara ilieleza kuwa serikali, kwa kushirikiana na mamlaka za mikoa, washirika wa kukabiliana na mlipuko huo pamoja na jamii za maeneo husika, inaendelea kutekeleza hatua za afya ya umma zinazolenga kukatiza mnyororo wa maambukizi na kulinda wananchi.

Timu za wataalamu walioko uwanjani zinafanya ufuatiliaji wa kitabibu, utoaji wa huduma kwa wagonjwa na ufuatiliaji wa watu waliokutana na waathirika.

Wizara imeisitiza kuwa hakuna amri ya kufunga shughuli mbali mbali iliyotolewa katika maeneo yaliyoathiriwa, wala hatua hiyo haipo katika mpango wa sasa. Wananchi wametakiwa kuepuka kusambaza taarifa zisizothibitishwa na kufuatilia taarifa kupitia njia rasmi za serikali.

Katika taarifa yake ya hivi karibuni kuhusu mlipuko huo iliyochapishwa Jumamosi, Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema kuwa hali ya maambukizi nchini DRC inaendelea kubadilika kwa kasi, huku idadi ya visa na ueneaji wa kijiografia vikiongezeka.

Mlipuko wa sasa umeeneza hofu kubwa kwani unasababishwa na kirusi adimu cha Bundibugyo, ambacho hakina chanjo au tiba iliyoidhinishwa, tofauti na kirusi cha “Zaire” (aina nyingine ya Ebola) kilichohusika katika milipuko 16 kati ya iliyowahi kutokea nchini Kongo hapo awali.