Wizara ya Mazingira Kenya kuwafurusha waishio pembezoni mwa mito
Waziri wa mazingira na maliasili wa Kenya, Aden Duale amesema kuwa serikali itaendeleza mpango wake wa kuwahamisha watu wanaoishi kando kando ya mito nchini humo.
Waziri Duale amesisitiza kuwa hii ni kwa maslahi ya wananchi kufuatia tishio la kutokea maafa na mafuriko ya mara kwa mara yanayosababisha kupasuka kingo za mito.
"Uhamishaji wa familia katika mito ya Nairobi ulikuwa wa halali, wa kibinadamu, na kwa manufaa ya wananchi kufuatia vifo vya watu kutokana na mafuriko jijini," amesema Duale.
Waziri huyo pia amesisitiza kuwa serikali itarejesha ardhi zote za umma katika maeneo nyeti na yenye chemchemi za maji.
Duale alikuwa akijibu maswali siku ya Jumanne mbele ya kamati maalumu ya bunge juu ya mazingira, misitu na mali asili.
Hii inaambatana na agizo la mapema mwezi Mei ambapo serikali ilitoa makataa ya siku mbili kwa wote wanaoishi kando kando ya mito kuhama takriban mita 30 kutoka kingo za mito. Mwezi huo karibu watu 180,000 walihamishwa kutoka makazi yao.
Hata hivyo mwezi Mei, zaidi ya watu 47 walifariki katika mojawapo ya mafuriko makubwa kuwahi kutokea Kenya kufuatia mabadiliko ya tabia nchi duniani.