AU yakabidhi kambi 6 za kijeshi kwa vikosi vya Somalia
(last modified Fri, 18 Oct 2024 02:51:42 GMT )
Oct 18, 2024 02:51 UTC
  • AU yakabidhi kambi 6 za kijeshi kwa vikosi vya Somalia

Kikosi cha Mpito cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (ATMIS) kimekabidhi rasmi kambi ya kijeshi ya Kuday kwa vikosi vya usalama vya Somalia, kuashiria hatua muhimu katika awamu ya tatu ya uondoaji wa wanajeshi hao wa kigeni.

ATMIS ilisema jana Alkhamisi kwamba, kambi ya Kuday, ambayo iko katika eneo la Lower Juba kusini mwa Somalia, imekuwa ikisimamiwa na Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) tangu 2015 na imekuwa na jukumu muhimu katika kulinda mji wa bandari wa Kismayo kama eneo la kimkakati.

Mkuu wa Kijeshi wa ATMIS, Mhandisi Suleiman Ibrahim amesema katika taarifa iliyotolewa huko Mogadishu, mji mkuu wa Somalia kwamba, "Makabidhiano haya yanadhihirisha uwezo wa serikali ya Somalia na nia ya kuendelea kuchukua majukumu ya usalama, ikiungwa mkono na ATMIS."

ATMIS hadi sasa imekabidhi kambi sita za kijeshi kwa vikosi vya usalama vya Somalia na kupunguza idadi ya wanajeshi kwa 2,000, kama sehemu ya uondoaji wa awamu ya tatu ulioidhinishwa na Umoja wa Mataifa na AU.

Jeshi la Somalia huku likiungwa mkono na wanamgambo kutoka maeneo mbalimbali ya nchi hiyo na washirika wao wa kimataifa limekuwa likiendesha oparesheni mbalimbali na mashambulizi ya kushtukiza dhidi ya al Shabaab tangu mwaka 2022. 

Somalia imekumbwa na hali ya mchafuko na ukosefu wa amani kwa miaka kadhaa sasa huku matishio makuu yakiwa ni kundi la al Shabaab na Daesh (ISIS). 

 

 

Tags