Maandamano Senegal kupinga jinai za Israel huko Lebanon na Gaza
(last modified Sun, 20 Oct 2024 04:47:24 GMT )
Oct 20, 2024 04:47 UTC
  • Maandamano Senegal kupinga jinai za Israel huko Lebanon na Gaza

Maandamano makubwa yamefanyika katika mji mkuu wa Senegal, Dakar, siku ya Jumamosi kupinga jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel huko Gaza na Lebanon.

Waandamanaji, wakiwemo wakimbizi wa Palestina na Lebanon wanaoishi Dakar, walipeperusha bendera na kubeba mabango ya kutaka amani. Waandamanaji walielezea wasiwasi wao kutokana na kuenea kwa mzozo huo hadi Lebanon na Yemen.

Maandamano hayo yalikuwa na mabango yanayoonyesha uharibifu mkubwa uliofanywa na Wazayuni huko Gaza. Waandamanaji walihimiza hatua madhubuti za kimataifa zichukuliwe kwa ajili ya kukomesha kupendelewa Israel katika vikao vya kimataifa.

Wakati huo huo wasanii wa Senegal wamechora jumbe za kuunga mkono Palestina na Lebanon kwenye kuta za Dakar huku wakibainisha kuchukizwa kwao na jinai za Israel.

Kundi la Wasanii Waafrika wa Michoro ya Kutani (RBS) na Kundi la Wasanii wa Kiafrika wa Kupambana na Ubaguzi wa Rangi wameshirikiana kuchora michoro kwenye barabara yenye shughuli nyingi zaidi katika kitongoji cha Ouakam ili kuongeza ufahamu kuhusu mashambulizi ya kinyama ya utawala haramu wa Israel huko Palestina na Lebanon.