UPSR: Afrika inajua kuwa BRICS imebadilisha mlingano wa jiopolitiki duniani
Kiongozi mwandamizi wa chama kimoja cha upinzani nchini Cameroon amesema jumuiya ya BRICS ni mbadala halisi wa kuleta mlingano kwenye jiopolitiki duniani na kusisitiza kwamba, nchi za Afrika zinaelewa fika suala hili.
Hayo yamesemwa na Serge Espoir Matomba, Katibu Kiongozi wa chama cha United People for Social Renovation cha Cameroon (UPSR) katika mahojiano na shirika la habari la Sputnik kitengo cha Afrika, pambizoni mwa mkutano wa BRICS unaofanyika huko Kazan nchini Russia.
Ameeleza bayana kuwa, "BRICS ni ulimwengu mwingine. Kwa maneno mengine, jumuiya hii inafafanua maana halisi ya ulimwengu wa pande nyingi."
Matomba amebainisha kuwa, "BRICS inasema lazima tusikilize kila mtu, tushirikiane na kila mtu, na tufanye mabadilishano na kila mtu, anapotaka, jinsi anavyotaka na mahala anapotaka."
Mwanasiasa huyo wa Cameroon amesisitiza kuwa, jumuiya ya kiuchumi ya BRICS imekuwa chanzo kikubwa cha motisha na hamasa kwa nchi nyingi za Afrika, kwa kuwa inazihimiza kupigania uhuru wao na kupinga ushawishi na ubeberu wa Magharibi.
Jumuiya ya Kiuchumi ya BRICS inaundwa na Brazil, Russia, India, China, Afrika Kusini, Iran, Misri, Ethiopia na Umoja wa Falme za Kiarabu. Nchi nyingi duniani zikiwemo za Afrika zimetuma maombi ya kujiunga na jumuiya hiyo.