Radi yaua na kujeruhi watu 48 kanisani, kaskazini mwa Uganda
(last modified Mon, 04 Nov 2024 06:27:55 GMT )
Nov 04, 2024 06:27 UTC
  • Radi yaua na kujeruhi watu 48 kanisani, kaskazini mwa Uganda

Watu 14 wamepoteza maisha na wengine 34 wamejeruhiwa baada ya radi kupiga kanisani wakati watu walipokuwa wamekusanyika humo kufanya maombi, kaskazini mwa Uganda.

Jeshi la Polisi la Uganda limethibitisha habari hiyo na kuongeza kuwa, radi hiyo ilipiga Jumamosi jioni katika kambi ya wakimbizi ya Palabek wakati watu walipokuwa wamesanyika kwa ibada.

Akitangaza habari hiyo, Msemaji wa Jeshi la Polisi, Rusoke Kituuma amesema: "Wahanga wa tukio hilo ambao hadi sasa wasifu wao bado haujatambuliwa, walikuwa wamekusanyika kanisani wakati mvua ilipoanza kunyesha saa 11 jioni juzi Jumamosi. Radi ilipiga milango ya saa 11:30 kwa saa za Uganda na kuua na kujeruhi watu 48. Wahanga hao walipelekwa kwenye Kituo cha Afya cha Paluda III baada ya tukio hilo." 

Kituuma aliandika hayo jana kwenye mtandao wa kijamii wa X na kuongeza kuwa, wengi wa watu wanaoishi kwenye kambi hiyo ya wakimbizi ni raia wa nchi jirani ya Sudan Kusini.

Tukio kama hilo la radi lilitokea pia mwezi Julai mwaka huu na ilipiga wilaya ya Nebbi ya kaskazini magharibi mwa Uganda na kujeruhi wanafunzi 77 waliokuwa wamekusanyika kwa mashindano ya michezo.

Mamlaka ya hali ya hewa Uganda imetoa tahadhari kuhusu radi, mafuriko na maporomoko ya ardhi katika baadhi ya maeneo ya milimani hasa katika msimu huu wa mvua unaoendelea hivi sasa.