Warundi waandamana kulaani 'hujuma' ya Rwanda
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i1186-warundi_waandamana_kulaani_'hujuma'_ya_rwanda
Katika kile kinachoonekana ni kuzidi kuharibika uhusiano kati ya Kigali na Bujumbura, maelfu ya wananchi wa Burundi wamefanya maandamano kuilaani Rwanda kwa kile wanachodai kuwa inafanya hujuma ya moja kwa moja dhidi ya nchi yao.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 13, 2016 11:57 UTC
  • Warundi waandamana kulaani 'hujuma' ya Rwanda

Katika kile kinachoonekana ni kuzidi kuharibika uhusiano kati ya Kigali na Bujumbura, maelfu ya wananchi wa Burundi wamefanya maandamano kuilaani Rwanda kwa kile wanachodai kuwa inafanya hujuma ya moja kwa moja dhidi ya nchi yao.

Waandamanaji hao ambao aghalabu yao walikuwa wafuasi wa chama tawala CNDD-FDD na muitifaki wake UPRONA, wamefanya maandamano katika mji mkuu, Bujumbura na maeneo mengine wakiilaani serikali ya Rais Paul Kagame wa Rwanda eti kwa kuyapa mafunzo makundi ya kihalifu yaliyoko katika kambi za wakimbizi zilizoko nchini Rwanda kwa lengo la kurudi nyumbani na kuiangusha serikali ya Rais Pierre Nkurunziza.

Hii ni katika hali ambayo, Rwanda imesema itaanza kukabidhi wakimbizi raia wa Burundi walioko nchini humo kwa nchi ambazo ziko tayari kuwapokea. Taarifa iliyotolewa jana Ijumaa na Ofisi ya Msemaji wa Serikali imesema kuwa, tayari serikali ya Kigali imeanza kufanya mazungumzo na washirika na jamii ya kimataifa kwa ujumla kuhusu namna ya kukabidhi wakimbizi wa Kirundi wapatao 75,000, kwa njia mwafaka na bila kuhatarisha usalama wao kwa nchi ambazo ziko tayari kuwapokea.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni na Msemaji wa serikali ya Rwanda, Loise Mushikiwabo amesema serikali ya Kigali imeshindwa kuhimili gharama za kuwadhaminia usalama na kuwatunza wakimbizi hao na kwamba uwepo wao nje ya nchi yao unazidi kulemaza juhudi za kuutafutia ufumbuzi mgogoro unaoikumba nchi yao. Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda alikanusha madai yaliyotolewa kwenye ripoti ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba nchi yake inatoa mafunzo ya kijeshi kwa wakimbizi wa Burundi ili waweze kuipindua serikali ya Rais Pierre Nkurunziza. Amesema Rwanda imekuwa ikiwapokea wakimbizi wa Burundi katika kalibu ya kutekeleza majukumu yake ya kimataifa na ujirani mwema na kwamba inasikitisha kuona Umoja wa Mataifa ukikosa kutambua juhudi hizo na badala yake kutoa madai ya uongo dhidi ya Kigali.