Lugha ya Kiswahili kuwa somo la lazima katika shule za msingi Uganda
Kituo cha Kitaifa cha Ukuzaji Mtaala (NCDC) nchinin Uganda kimetangaza kuwa lugha ya Kiswahili itaanzishwa kama somo la lazima katika shule za msingi kwa awamu kuanzia mwaka ujao 2025.
Grace Baguma, mkurugenzi wa NCDC amesema kuwa, uzinduzi utaanza magharibi mwa Uganda, haswa katika Jiji la Fort Portal, na wilaya za Kasese na Kabarole.
Bi Baguma alieleza kuwa ingawa Baraza la Mawaziri liliidhinisha ufundishaji wa lazima wa Kiswahili katika shule zote za msingi nchini kote mwaka wa 2022, rasilimali chache zimechelewesha kkutekelezwa mpango huo kote nchini.
"Tunaanza na shule za magharibi mwa Uganda kwa sababu ya uhaba wa kifedha, kwa kuwa tunategemea fedha za serikali kwa usambazaji," amesema alipokuwa akiwahutubia walimu wa shule za msingi wanaopata mafunzo ya mtaala mpya wa Kiswahili katika Chuo cha Ualimu cha Msingi cha Canon Apollo Core.
Kiswahili ni kati ya lugha 10 zinazozungumzwa na watu wengi zaidi duniani, ikiwa na wazungumzaji zaidi ya milioni 200.
Ni lugha iliyoenea zaidi pia katika nchi za Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika na pia katika nchi za Asia Magharibi.