Watu 3 wauawa katika shambulizi la wanaotaka kujitenga nchini Cameroon
(last modified Tue, 19 Nov 2024 10:49:35 GMT )
Nov 19, 2024 10:49 UTC
  • Watu 3 wauawa katika shambulizi la wanaotaka kujitenga nchini Cameroon

Takriban watu watatu yaani mwanajeshi mmoja na raia wawili wameuawa katika shambulio la watu wanaotaka kujitenga kwenye eneo linalotokea vita vya mara kwa mara la kaskazini magharibi mwa Cameroon.

Duru za kuaminika za ndani ya Cameroon zimethibitisha habari hiyo na kutangaza kuwa, watu hao waliouawa walikuwa kwenye gari katika barabara ya Ndu-Foumban wakati wapiganaji wanaotaka kujitenga na serikali kuu walipowavizia na kuwashambulia.

Sehemu moja ya taarifa ya duru hizo za usalama imesema: "Raia waliouawa walikuwa wameomba lifti kutoka kwa mwanajeshi huyo. Njiani, watu wanaotaka kujitenga waliokuwa wamejificha msituni walilifyatulia risasi gari hilo na kuwaua watu watatu na kuwajeruhi wengine wawili."

Wanajeshi wa ziada wametumwa kwenye barabara hiyo ambayo mara kwa mara inashuhudia mashambulizi ya watu wenye silaha.

Uasi wa watu wanaotaka kujitenga umekuwa ukiendelea katika maeneo mawili yanayozungumza lugha ya Kiingereza huko kaskazini magharibi na kusini magharibi mwa Cameroon tangu mwaka 2017.

Watu hao ambao mara nyingi wanaendesha mashambulizi ya kuvizia, wanataka kujitenga na maeneo ya Cameroon yanayozungumza lugha ya Kifaransa. Wanataka kuunda nchi huru katika maeneo yanayozungumza Kiingereza ya kaskazini magharibi na kusini magharibi mwa nchi hiyo.

Cha kustaajabisha ni kwamba, pande hizo zinapigana na kumwaga damu zao kwa sababu ya lugha tu tena lugha za kikoloni za Kifaransa na Kiingereza, wakoloni ambao wanaendelea kuzisababishia maafa makubwa nchi za Afrika.