Femi Fani Kayode: Mataifa ya Afrika yanapaswaa kuvunja uhusiano na Israel
Waziri wa zamani wa Usafiri wa Anga nchini Nigeria na kiongozi wa Kikristo nchini humo amezitaka nchi za Kiafrika kuvunja uhusiano wa kidiplomasia na utawala ghasibu wa Israel ili kuwashinikiza Wazayuni wakomeshe mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Palestina na Lebanon.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na mwandishi wa habari wa Iran Press mjini Abuja, Femi Fani Kayode ameusifu Mhimili wa Muqawama akisema kuwa Iran, Hamas, Islamic Jihad, Hizbullah, Iraqi PMF, na Ansarullah wa Yemen wanapaswa kupewa jina la "Mhimili wa Uhuru."
"Mhimili wa Muqawama unapigana kwa ajili ya kulinda Mashariki ya Kati yote, na ni kawaida kwa watu na tawala kujilinda na kupinga maovu", amesema Fani Kayode na kuongeza kuwa: Mnakabiliana na dola lililozama katika kuua kila mtu kandokando yake. Waliua sana wakati wa Nakba. Kwa hiyo, Mhimili wa Muqawama (Axis of Resistance) unasema: "imetosha", na umesimama kukabiliana na makatili hao.
Waziri wa zamani wa Usafiri wa Anga wa Nigeria amesema: "Mhimili wa Muqawama ni Mhimili wa Uhuru. Hawa ni watu wanaojaribu kila wawezalo kuhakikisha kwamba uhuru wanaopigania sio tu kwa Wapalestina bali Mashariki ya Kati yote."
Femi Fani Kayode amesema: "Wazayuni wanakandamiza kila mtu wakiwemo Wakristo na Waislamu kwa kutumia fikra na itikadi za kutisha. Fikra hizo mbaya zina nia ya kuanzishwa Israel kubwa ambayo mpaka wake unaanzia kwenye mipaka ya Misri na kuelekea kwenye mipaka ya Iran."
Ameongeza kuwa: "Nadhani kwamba tunapaswa kuwapongeza wale wanaopinga uovu huu. Wanamuqawama wamesema hapana kwa uovu huu na wanapinga mauaji ya kimbari, na sisi tunawaunga mkono wale wanaopinga mauaji ya kimbari."