Maelfu ya Watunisia wakaribisha kutolewa hati ya kukamatwa Netanyahu
(last modified Sat, 23 Nov 2024 07:56:15 GMT )
Nov 23, 2024 07:56 UTC
  • Maelfu ya Watunisia wakaribisha kutolewa hati ya kukamatwa Netanyahu

Maelfu ya wananchi wa Tunisia wamefanya maandamano katika mji mkuu wa nchi hiyo wakipongeza na kukaribisha kutolewa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) hati ya kukamatwa Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni Benjamin Netanyahu na aliyekuwa Waziri wa Ulinzi wa utawala huo Yoav Gallant.

Siku ya Alhamisi, Novemba 21, Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC)  yenye makao yake makuu mjini The Hague ilitoa hati ya kukamatwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na waziri wa zamani wa vita Yoav Galant kwa tuhuma za uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya binadamu na kutumia njaa kama silaha dhidi ya watu wa Gaza.

Wananchi wa Tunisia walioshiriki katika maandamano hayo hapo jana, yaliyofanyika kwa wito wa Jumuiya ya Waungaji mkono wa Palestina nchini Tunisia ili kuonyesha mshikamano na watu wa Gaza, walibeba maberamu yaliyoandikwa "kwa nini dunia iko kimya dhidi ya Netanyahu? na  "Tutaiokoa Palestina kwa roho zetu na damu zetu".

Mohammed Al-Bashir Khezri, Mkurugenzi Mtendaji wa Jumuiya ya Waungaji Mkono wa Palestina nchini Tunisia amesema kuwa: "Uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai umeonyesha kuwa licha ya pingamizi za Marekani na baadhi ya waungaji mkono wa utawala wa Kizayuni, kuna sauti ya haki duniani ambayo haijafifia.

Kuhusiana na suala hilo, maelfu ya wananchi wa Mauritania nao pia wamejitokeza kwa wingi mabarabarani wakipongeza hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, ambapo sambamba na kutangaza kuchukizwa kwao na serikali za Kiarabu kwa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni, wametangaza uungaji mkono wao kwa Mhimili wa Muqawama.

Waandamanaji wametoa wito kwa wananchi wa nchi za Kiarabu kuungana ili kuunga mkono haki za Wapalestina na kukabiliana na siasa za ukaliaji ardhi kwa mabavu na za ubaguzi wa rangi za utawala wa Kizayuni.