Wananchi wa Namibia wamepiga kura katika uchaguzi wa rais, wabunge
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i119420-wananchi_wa_namibia_wamepiga_kura_katika_uchaguzi_wa_rais_wabunge
Wananchi wa Namibia wamejitokeza kwa wingi katika  vituo vya kupigia kura leo  Jumatano kumchagua rais ajaye wa taifa hilo la kusini mwa Afrika pamoja na wabunge 104.
(last modified 2024-11-27T10:03:00+00:00 )
Nov 27, 2024 10:03 UTC
  • Wananchi wa Namibia wamepiga kura katika uchaguzi wa rais, wabunge

Wananchi wa Namibia wamejitokeza kwa wingi katika  vituo vya kupigia kura leo  Jumatano kumchagua rais ajaye wa taifa hilo la kusini mwa Afrika pamoja na wabunge 104.

Netumbo Nandi-Ndaitwah, 72, makamu wa rais wa sasa, ndiye mgombea urais wa chama tawala cha South West Africa People's Organization (SWAPO), ambacho kimekuwa madarakani kwa miaka 34.

Kuna wapiga kura milioni 1.4 waliojiandikisha katika nchi hiyo kubwa lakini yenye idadi ndogo ya watu milioni 3.

Vyama 15 vya kisiasa vinachuana kuwania nafasi ya rais na vile vile viti katika Bunge la Kitaifa. Ikiwa Nandi-Ndaitwah atashinda uchaguzi, atakuwa rais wa kwanza mwanamke wa Namibia.

Wapinzani wakuu wa Nandi-Ndaitwah ni pamoja na Panduleni Itula wa chama cha IPC, ambaye alifanikiwa kupata asilimia 29.4 ya kura katika uchaguzi wa 2019, ambapo alishindana na hayati Rais Hage Geingob, ambaye alipata asilimia 56.3 ya kura, na kushuka kutoka asilimia 87 ambayo alishinda wakati wa muhula wake wa kwanza mnamo 2014.