Matokeo yanasubiriwa Namibia baada ya uchaguzi wenye ushindani mkali
Shughuli ya kuhesabu kura inaendelea nchini Namibia baada ya uchaguzi ulioonekana kuwa na ushindani mkali zaidi katika miongo kadhaa.
Kulikuwa na misururu mirefu nje ya vituo vya kupigia kura siku nzima ya Jumatano huku vijana wa nchi hiyo wakipiga kura ya kumtafuta rais mpya na wabunge.
Upigaji kura ulifungwa saa tisa jioni kwa saa za huko na takwimu za awali zinaonyesha kulikuwa na idadi kubwa ya wapiga kura walioshiriki zoezi hilo.
Chama tawala, SWAPO, ambacho kimeitawala Namibia tangu nchi hiyo ipate uhuru wake kutoka kwa utawala wa kibaguzi wa Afrika Kusini mwaka 1990, kimekabiliwa na ushindani mkubwa katika uchaguzi wa mwaka huu.
Iwapo chama cha SWAPO kitapata ushindi, mgombea wake wa urais, Makamu wa Rais Netumbo Nandi-Ndaitwah, atakuwa rais wa kwanza mwanamke nchini humo.
Hata hivyo katika kuelekea uchaguzi huo, wachambuzi walisema kuna uwezekano mkubwa kuwa SWAPO inaweza kuondolewa madarakani na vijana ambao ni asilimia 64 ya wapiga kura waliojiandikisha.
Inadaiwa kuwa vijana wamechoshwa na viwango vya juu vya ukosefu wa ajira, ukosefu wa usawa na madai ya ufisadi, hivyo wanataka mabadiliko.
Ili kuchaguliwa kuwa rais, mgombea lazima apate zaidi ya asilimia 50 ya kura la sivyo kutakuwa na duru ya pili ya uchaguzi. Matokeo yanatarajiwa kutangazwa kufikia wikendi hii.