Somalia na Jubaland zatoa waranti wa kukamatwa marais wa pande hizo mbili
Serikali ya Shirikisho la Somalia imetoa waranti wa kukamatwa Rais wa Jimbo la Jubaland katika kile kinachoweza kuonekana kuwa ni hatua ya kujibu uamuzi wa huko nyuma wa Jaji wa Jubaland aliyetoa waranti wa kukamatwa Rais Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia.
Rais Ahmed Mohamed Islam Madobe anaongoza Jubaland na hivi karibuni ameingia kwenye mgogoro mkubwa na Somalia akitaka Jubaland ijitenge na ardhi nyingine ya nchi hiyo.
Jimbo la Jubaland ni moja ya majimbo matano ya Somalia yenye utawala wa ndani na hivi karibuni lilifanya uchaguzi ambapo Madobe alitangazwa mshindi kuliongoza jimbo hilo kwa muhula wa tatu mfululizo.
Somalia inamshutumu Madobe kuwa ni muhaini ikidai kuwa anafichua taarifa za siri kwa mashirika ya kigeni.
Kwa upande wake, Jubaland inamtuhumu Rais wa Somalia kwa uhaini ikidai kuwa anachochea vita vya wenyewe kwa wenyewe na kuandaa mazingira ya uasi wa silaha ili aweze kupata fursa ya kupindisha katiba ya nchi hiyo.
Serikali ya Shirikisho ya Somalia inadai kuwa uchaguzi wa Jubaland umefanyika bila ya kuishirikisha serikali kuu, hivyo utaendelea kuwa ni uchaguzi haramu.
Mapema wiki hii Jamhuri ya Shirikisho la Somalia ilituma wanajeshi wa ziada huko Jubaland kukabiliana na uchaguzi huo.
Mapigano baina ya mawakala wa uchaguzi yaliripotiwa sana katika maandalizi ya zoezi hilo la uchaguzi la hivi karibuni huko Jubaland.
Inasemekana kuwa Rais wa serikali ya Jubaland ni mshirika wa Kenya huku serikali za Somalia na Ethiopia zikidaiwa kuwaunga mkono wapinzani wake.