Watu 30 wahofiwa kufa kwenye maporomoko ya ardhi Uganda
Takribani watu 30 wanahofiwa kufa kufuatia maporomoko ya ardhi katika kijiji kimoja mashariki mwa Uganda. Hayo yamelezwa na afisa mmoja wa eneo hilo aliyeonya kuwa idadi hiyo huenda ikaongezeka.
Msemaji wa Shirika la Msalaba Mwekundu la Uganda John Cliff Wamala amesema kuwa, miili 13 imepatikana. Amesema zaidi ya nyumba 40 zimeharibiwa kabisa. Ofisi ya Waziri Mkuu wa Uganda ilitoa tahadhari, ikiandika kwenye mtandao wa X kuwa mvua kubwa iliyonyesha juzi Jumatano katika maeneo tofauti ya Uganda ilisababisha maafa katika maeneo mengi.
Operesheni ya uokoaji inaendelea, Shirika la Msalaba Mwekundu la Uganda lilisema katika taarifa fupi kwenye mtandao wa kijamii wa X.
Kulingana na gazeti la Daily Monitor la Uganda ni kuwa, mili mingi iliyopatikana ni ya watoto huku makumi ya watu wakiwa bado hawajulikani waliko.
Siku ya Jumatano, Ofisi ya Waziri Mkuu ilitoa onyo la maafa kupitia taarifa yake kwenye mtandao wa kijamii wa X.
Kingo za mito zimepasuka, shule na makanisa zimefurika na kuharibu madaraja, na kuwatenga watu wengi. Wanajeshi wametumwa kusaidia katika juhudi za utafutaji na uokoaji.
Uganda imekuwa ikikumbwa na matukio kama haya mara kwa mara ambapo Agosti mwaka huu watu zaidi ya 20 walipoteza maisha yao katika janga la kuporomoka kwa jaa la takataka mjini Kampala.